Waziri Mkuu mgeni rasmi maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani

NA GODFREY NNKO

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ambayo yatafanyika kitaifa jijini Arusha.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Rodney Thadeus ameyasema hayo leo Aprili 24,2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.

"Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Kassim Majaliwa."

Amesema,sherehe na mikutano itakayoanza Aprili 27 na 28,2025 ni sehemu ya shughuli za kuelekea kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika Aprili 29,2025 katika Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha.

Thadeus amesema, kwa mwaka huu wizara hiyo kupitia Idara ya Habari-Maelezo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Umoja wa Mataifa (UN), washirika wa maendeleo,

Waandishi wa habari, vyombo vya habari vya mtandaoni na nje ya mtandao,mashirika ya kiraia na watetezi wa haki za binadamu,

Pia watafiti,wasomi na wadau mbalimbali wa habari wakiongozwa na Jamii Afrika ambaye ni mwenyekiti kwa mwaka huu wameandaa maadhimisho ya siku tatu katika kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo amesema kwa mwaka huu ni Uhabarishaji kwenye Dunia Mpya:Mchango wa Akili Unde kwenye Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Amesema,kaulimbiu hiyo inagusa masuala muhimu yanayohusiana na mabadiliko ya teknolojia na athari za akili unde katika uandishi wa habari na vyombo vya habari.

"Kaulimbiu hii inatufundisha kuhusu Ulimwengu mpya wa habari unaoendeshwa na akili mnemba ambapo vyombo vya habari vinahitajika kuwa makini na kutumia teknolojia hii kwa manufaa ya jamii."
Vilevile amesema, kaulimbiu hiyo inatoa changamoto kwa waandishi,wamiliki wa vyombo vya habari na Serikali kuhakikisha teknolojia hiyo inasaidia badala ya kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya watu kupata habari sahihi.

Wakati huo huo, Serikali imesema maadhimisho hayo yatatoa nafasi kwa wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kujadili masuala yanayohusu uhuru wa vyombo vya habari.

Mambo mengine ni kuhusu changamoto zinazohusiana na teknolojia na mchango wa akili unde katika uhuru wa vyombo vya habari.

"Na zimeandaliwa mada mbalimbali ambazo zitajadiliwa katika matukio na mikutano ya makundi tofauti tofauti.

"Pia,kutakuwa na maonesho ambapo pamoja na mambo mengine yataonyesha bidhaa za maarifa, michoro na ubunifu unaohusiana na ujuzi wa vyombo vya habari."

Mambo mengine amesema ni kuhusu utafiti,mabadiliko ya kidijitali na uhuru wa kisanii kwa kutumia akili unde.

Ameongeza kuwa,siku ya huru wa vyombo vya habari duniani itatumika kama fursa ya kuweka mkazo mkubwa katika uhuru wa kujieleza ndani ya ajenda ya jumla ya haki za binadamu.

UN

Kwa upande wake,Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania,Susan Ngongi Namondo amesema, uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari katika kutekeleza majukumu yao ni msingi muhimu katika kukuza demokrasia, maendeleo na ustawi bora wa jamii kwa ujumla.
Amesema, katika maadhimisho hayo jijini Arusha yatawapa wadau mbalimbali uwanda mpana wa kujadili, kutafakari na kushauri hasa kuhusu matumizi ya akili unde ili kuhakikisha inakuwa na manufaa kwa sekta ya habari na jamii.

Pia, Namondo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuimarisha na kudumisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Ameongeza kuwa,vyombo huru vya habari na uhuru wa wanahabari katika kutekeleza majukumu yao ni msingi muhimu wa kufurahia haki nyingine zote za binadamu ikiwemo utawala bora.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo Machi 3 huwa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari kwa kunogeshwa na kauli mbiu ambapo kwa mwaka 2024 iliangazia “Uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news