DAR-Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande ameongoza uwakilishi wa wizara na taasisi zake katika hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuchangia Kongamano la E-Learning Africa 2025 litakaloyaleta pamoja makundi 1,500.
Sambamba na Mawaziri 50 kutoka baranı Afrika wanaotarajia kushiriki Kongamano hilo litakalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) tarehe 7 hadi 9 mwezi Mei, 2025.
Mgeni rasmi atakayefungua Kongamano hilo anatarajiwa kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufungwa na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Tukio hilo lililolenga kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 1, limemshirikisha pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba.
Vilevile wakuu wa taasisi 19 wa Wizara ya Fedha ikiwemo TRA, CMSA, TCB, PPRA, GPSA, TIRA, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), NBS), Chuo cha Mipango, PPRA, TIA, IFM, TADB, PSPTB, UTT-AMIS, Chuo cha Takwimu cha Afrika Mashariki na NIC.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt.Natu El-Maamry Mwamba, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Bw. Justine Japhet, aliutangazia Umma kwamba, Wizara ya Fedha na Taasisi zake, imechangia shilingi milioni 466 na kufanya jumla ya kiasi cha fedha zote kilichochangwa usiku huo kufikia shilingi bilioni 1.569.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, katika tukio hilo lililofayika katika Hotel ya Hyatt jjjini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, aliyataja baadhi ya mafanio ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo kuwa ni pamoja na kubaini mikakati na mbinu mpya za kuongeza matumizi ya teknolojia za kidijitali.
Ni katika elimu na sekta nyingine, kuvutia programu za pamoja ikiwemo bunifu na teknolojia zinazoibuliwa nchini.
Manufaa mengine ni kuvutia kampuni za teknolojia za kikanda na kimataifa kuja kuwekeza nchini, kuimarisha ubia kati ya sekta za umma na binafsi katika maendeleo na matumizi ya teknolojia za kidijitali.Aidha,kuchagiza uchumi wa ndani kupitia bidhaa na huduma zitakazotolewa kwa washiriki wa kongamano, na kuhamasisha washiriki wa Kongamano kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini.











