Afrika tuzalishe ujuzi utakaosaidia kukuza uchumi-Mheshimiwa Mbeki

NA GODFREY NNKO

VIONGOZI wa Bara la Afrika wametakiwa kuweka mikakati thabiti ambayo itawezesha mataifa yao kuzalisha ujuzi utakaosaidia kukuza uchumi kwa jamii na bara lote kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo Mei 24,2025 na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki katika Mhadhara wa 15 wa Siku ya Afrika ya Thabo Mbeki (The Thabo Mbeki 15th Africa Day Lecture) uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mbeki amesisitiza kuwa,ni bora Afrika iwe na ujuzi wa hali ya juu kutoka ndani ya bara lenyewe badala ya kutegemea wataalamu kutoka nje.

Ameongeza kuwa,Afrika ina uwezo na wasomi wa kutosha kushughulikia changamoto zinazolikabili bara hilo bila kutegemea usaidizi kutoka upande wa pili.

Vilevile amesisitiza umuhimu wa viongozi wenye shauku na ari ya kutekeleza sera zilizopo barani Afrika ili zilete matokeo bora. 

Amesema, bara la Afrika lina sera na mikakati mizuri, ingawa changamoto inajitokeza pale ambapo viongozi hawana nia thabiti ya kuzitekeleza ili zilete matunda.

Mhadhara wa Siku ya Afrika ya Thabo Mbeki ni tukio la kila mwaka linaloandaliwa na Thabo Mbeki Foundation (TMF) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (Unisa) kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Afrika.

Ni siku ambayo huadhimisha kuanzishwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU) Mei 25, 1963, huko Addis Ababa, Ethiopia.

Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 62 tangu kuanzishwa kwa OAU, ambayo ndiyo chimbuko la Umoja wa Afrika (AU) uliozinduliwa rasmi huko Durban, Afrika Kusini mwaka 2002.

Uamuzi wa kuandaa Mhadhara wa 15 wa Siku ya Afrika ya Thabo Mbeki nchini Tanzania mwaka huu unatokana na mchango mkubwa wa Tanzania katika historia ya Bara la Afrika ukiwa umejengwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wakfu wa Thabo Mbeki kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo walikuwa wenyeji wa mhadhara huo wa kila mwaka wa Siku ya Afrika.

Mhadhara huo umewaleta pamoja viongozi na wadau kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika ili kutafakari maendeleo ya bara na mustakabali wake kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news