ATCL yatoa tahadhari kwa umma kuhusu tiketi bandia

DAR-Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imepokea taarifa kutoka kwa watu mbalimbali waliojitambulisha kuwa miongoni mwa wafanyabiashara kutoka Kariakoo, waliokatiwa tiketi za safari na wakala anayeitwa Space Travel, mwenye ofisi katika eneo la Kariakoo, anayetambulika kwa jina la Yasmin Ladha.

Abiria hao waliwasilisha malalamiko yao kwa ATCL wakieleza wasiwasi juu ya tiketi zao za kurejea kutoka Guangzhou, China, baada ya kuarifiwa na wakala huyo kuwa ndege za ATCL hazikuwa na nafasi kwa tarehe walizopanga kurudi.

Kufuatia malalamiko hayo, ATCL ilichukua hatua za haraka kufanya uhakiki wa tiketi husika katika mfumo wake na kubaini kuwa majina ya abiria hao hayakuwepo kwenye orodha ya waliopaswa kusafiri kwa tarehe walizotaja.

Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa abiria walikatiwa tiketi halali za kwenda Guangzhou na kampuni ya Space Travel, ambayo ilitumia huduma za wakala aliyesajiliwa kwenye mfumo wa “Global Distribution System” (GDS), yaani Satguru Travel & Tour Services (JMD). Hata hivyo, iligundulika kuwa Space Travel alihusika kutengeneza tiketi bandia za kurudi.

Katika kushughulikia changamoto hii, abiria wote 32 waliokumbwa na tatizo hilo walifanikiwa kulipia tiketi mpya ATCL na waliweza kusafiri kwa tarehe walizopendelea.

ATCL itaendelea kuwahudumia abiria wengine watakaohitaji kununua tiketi zao kupitia mwakilishi wake aliyepo Guangzhou, China.

Kufuatia udanganyifu huu, ATCL imechukua hatua ya kuwasiliana na ofisi za GDS pamoja na mawakala wote wanaofanya biashara na Space Travel na kuwaelekeza kusitisha mara moja uuzaji wa tiketi kupitia wakala huyo kuanzia tarehe 28 Aprili 2025.

Hatua hii imelenga kulinda usalama na maslahi ya watumiaji wa huduma za usafiri wa anga, huku taratibu nyingine za kisheria dhidi ya Space Travel zikiendelea kuchukuliwa.

ATCL inapenda kuwahimiza wateja wake kununua tiketi kupitia Aplikesheni ya Simu ya Air Tanzania, Tovuti yetu rasmi: www.airtanzania.co.tz, Kituo chetu cha huduma kwa wateja ‪(+255 748 773 900‬,) kinachopatikana masaa 24 kila siku au kwa kutembelea moja kwa moja Ofisi za ATCL. Iwapo mteja atachagua kununua tiketi kwa wakala, ni wajibu wa mteja kuhakikisha kuwa tiketi aliyopatiwa inatambulika kwenye mfumo rasmi wa ATCL.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news