NA DIRAMAKINI
WAZIRI wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega amesema kuwa,wizara hiyo kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Wizara ya inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 37,435.04.
Kati ya hizo kilometa 12,527.44,Mheshimiwa Ulega amesema ni barabara kuu na kilometa 24,907.60 ni barabara za mikoa.
Ameyasema hayo leo Mei 5,2025 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
“Katika mwaka wa fedha 2024/25, miradi ya barabara kuu iliyopangwa kutekelezwa ni ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa kilometa 385, ukarabati wa kilometa 35 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa madaraja 17, ukarabati wa daraja moja,maandalizi ya ujenzi wa madaraja tisa na Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa madaraja mawili.”
Waziri huyo amesema,hadi kufikia Aprili, 2025,ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa kilometa 109.49 umekamilika na ujenzi wa kilometa 275.51 unaendelea.
Kwa upande wa madaraja, Waziri Ulega amesema,ujenzi wa madaraja Matano unaendelea na ujenzi wa madaraja Matano upo katika hatua za maandalizi.
Vilevile, amesema taratibu za ununuzi ya Makandarasi wa ujenzi wa madaraja matano zinaendelea. “Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa madaraja 11 na ukarabati wa daraja mpja katika mikoa mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa, miradi ya barabara za mikoa iliyopangwa kutekelezwa ni ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa kilometa 98,ukarabati kwa kiwango cha changarawe wa barabara zenye urefu wa kilometa 925 pamoja na ujenzi na ukarabati wa madaraja na makalavati 107.
Hadi Aprili, 2025 amesema jumla ya kilometa 98.13 za barabara za mikoa zilijengwa kwa kiwango cha lami na jumla ya kilometa 192.9 zilikarabatiwa kwa kiwango cha changarawe.
Pia, amesema ujenzi na ukarabati wa madaraja madogo saba kwa kutumia fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali na tisa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara umekamilika na
madaraja 91 yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Awali Waziri Ulega amelieleza Bunge kuwa,katika mwaka wa fedha 2024/25, Wizara ya Ujenzi ilitengewa Shilingi 81,407,438,000.00 ikiwa ni Bajeti ya Matumizi ya
Kawaida.
Kati ya fedha hizo, Shilingi 76,588,233,000.00 ilikuwa ni Bajeti ya Mishahara na Shilingi 4,819,205,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo.
Vilevile amesema hadi Aprili, 2025 jumla ya Shilingi 63,506,309,562.24 zilipokelewa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 61,152,975,329.92 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Wizara na Taasisi na Shilingi 2,353,334,232.32 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo ya Wizara na Taasisi zake.
Amesema,Bajeti kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo iliyotengwa kwa mwaka wa fedha
2024/25 kwa Wizara ya Ujenzi ni Shilingi 1,687,888,714,000.00.
Kati ya fedha hizo, Shilingi 1,141,803,989,000.00 ni fedha za ndani na Shilingi 546,084,725,000.00 ni fedha za nje.
Ulega amesema,kati ya fedha za ndani, Shilingi 599,756,467,800.00 ni fedha zilizotengwa kwa ajili ya bajeti ya Mfuko wa Barabara na Shilingi 542,047,521,200.00 ni fedha kutoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
"Hadi Aprili, 2025 fedha zilizopokelewa ni Shilingi 1,535,092,021,470.55. Kati ya fedha hizi, Shilingi 944,881,583,335.76 ni fedha za ndani na Shilingi 590,210,438,134.79 ni fedha za nje.
"Kati ya fedha za ndani zilizopokelewa, Shilingi 482,085,328,011.98 ni kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali na Shilingi 462,796,255,323.78 ni za Mfuko wa Barabara."..SOMA KWA KINA HAPA
