MHESHIMIWA Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyochambua utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi ya mwaka wa fedha 2024/25, ninaomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea na kujadili Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Aidha,ninaliomba Bunge lako Tukufu liridhie kupitisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/26.
2. Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kukutana leo hii hapa Bungeni.
3. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii adhimu, na kwa unyenyekevu mkubwa, kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini, na kuniteua kuwa Waziri wa Ujenzi tangu tarehe 08 Desemba, 2024.
Naomba kupitia kwako nimuahidi Mheshimiwa Rais kuwa, kwa kushirikiana na watendaji wenzangu katika Wizara, nitatekeleza majukumu haya niliyopewa kwa uaminifu na moyo wa uzalendo.
4. Mheshimiwa Spika, sambamba na shukrani hizo kwa Mheshimiwa Rais, kipekee nitumie fursa hii kumpongeza kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya ya kuliongoza Taifa letu. Sote ni mashuhuda wa namna alivyofanya mapinduzi makubwa katika sekta zote nchini.
Chini ya uongozi wake tumeshuhudia miradi mikubwa, katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya ujenzi inavyoendelea kutekelezwa nchi nzima.
Kukamilika kwa miradi hii kunachochea maendeleo ya sekta nyingine za kiuchumi na kijamii na hivyo kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Hakika Watanzania tunajivunia na tunatembea kifua mbele chini ya uongozi imara wa Mheshimiwa Rais.
5. Mheshimiwa Spika, naomba kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdory Mpango, Makamu wa Rais; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu na Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb.),Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumsaidia na kumshauri vyema Mheshimiwa Rais katika uongozi wa nchi yetu.
Viongozi hawa pia wamekuwa wakitoa miongozo na maelekezo mbalimbali ambayo yamesaidia sana katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ujenzi. Nawashukuru sana.
6. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kukupongeza wewe binafsi pamoja na Naibu Spika kwa namna mnavyoongoza kwa weledi Bunge hili la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo litafikia tamati katika Mkutano huu.
Aidha, nitumie nafasi hii kutoa shukrani kwa Ofisi yako, Katibu wa Bunge na watendaji wa Ofisi ya Bunge kwa ushirikiano ambao mmetupatia wakati wote katika utekelezaji wa majukumu yetu.
7. Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso (Mb.) na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Anne Kilango Malecela (Mb.).
Kamati hii imekuwa bega kwa bega na Wizara katika utekelezaji wa majukumu yake kupitia maelekezo, maoni na ushauri katika masuala mbalimbali.
Hali kadhalika, Kamati hii ilifanya uchambuzi wa kina wa Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kutoa ushauri ambao umezingatiwa katika bajeti hii ninayoisoma mbele ya Bunge lako.
8. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kutoa mkono wa pole kwako wewe binafsi, Mheshimiwa Spika, Bunge lako, Chama cha Mapinduzi, wananchi wa Jimbo la Kigamboni, marafiki na familia, kufuatia kifo cha Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigamboni. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.
9. Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 16 Novemba, 2024, yalitokea maafa makubwa kutokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne katika eneo la Kariakoo Jijini Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilisababisha vifo, majeruhi pamoja na upotevu wa mali. Nitumie nafasi hii kutoa pole kwa wote walioathirika na maafa haya, na ninawaombea marehemu wote wapumzike kwa amani.
Wizara yangu, ikiwa ni msimamizi wa shughuli za majenzi nchini, inaendelea na taratibu za kutunga Sheria ya Majengo kwa ajili ya kusimamia Sekta ndogo ya Majengo nchini. Sheria hii itakapoanza kutumika itakuwa muarobaini wa changamoto zilizopo hususan katika masuala ya uratibu, usimamizi na udhibiti wa sekta hiyo hapa nchini.
10. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kwa mara nyingine kutoa pole kwa wananchi kutokana na adha iliyotokea baada ya daraja la dharura la Somanga Mtama kukatika na kusababisha changamoto ya mawasiliano baina ya mkoa wa Pwani na Mikoa ya Kusini.
Daraja hili lipo katika eneo linapojengwa daraja jipya la kudumu katika mpango wa matengenezo yanayoendelea kufuatia uharibifu uliotokea mwaka jana kutokana na mvua za El-nino na Kimbunga Hidaya.
Aidha, nitoe pole kwa wananchi katika maeneo
mengine nchini yaliyoathirika kutokana na uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja.
Niwaondoe hofu na kuwapa matumaini wananchi kuwa Serikali, chini ya Mheshimiwa Rais, Daktari Samia Suluhu Hassan ipo kazini mchana na usiku ili kurejesha mawasiliano katika hali yake ya kawaida kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
11. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, niruhusu sasa nitoe taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26.