Ibraah aachiwa huru kutoka Konde Gang Music Worldwide

DAR-Afisa Mtendaji Mkuu wa Harmonize Entertainment Limited, Rajab Abdul Kahali (Harmonize) kupitia Lebo ya Konde Gang Music Worldwide imemsamehe mwanamuziki wake Ibrahim Abdallah (Ibraah) kiasi cha shilingi bilioni 1 ambacho alipaswa kulipa kulingana na masharti ya mkataba.
Mei 15,2025 Harmonize amempatia baraka zake rasmi Ibraah ili kuanza kujitegemea kama msanii huru ambaye si mwana chama tena wa lebo hiyo.

“Nikiri kwamba mdogo wangu alinitumia meseji na kuniomba kwamba anataka kutoka kwenye lebo na kwenda kujitegemea nami nilimjibu moja kwa moja kwamba nakutakia kila la kheri.

"Kaa chini na viongozi wa Konde Gang soma mkataba wako muone mnafanyaje, mkataba unasema endapo atataka kuvunja mkataba na kumiliki nyimbo zote hata zile alizozifanya na mimi ili ziwe zake milele ziwe zinaingiza kwake inatakiwa alipie hicho kiasi cha pesa kilichotajwa miaka minne iliyopita.

“Hayo ndio yalikuwa mazungumzo,sijui nini kimetokea kwake baadae akaja kusema kwenye mitandao yake kwamba nimemdai kiasi cha shilingi bilioni moja.

"Nikiri kwamba sijamdai kiasi cha bilioni moja na nisingependa pesa yangu tena ije kunichafua mwenyewe, namtakia kila la kheri, kuanzia sasa yeye ni msanii anayejitegemea promoters mkiwa na show muiteni apate riziki aisaidie familia yake.

“Kuhusu kauli yake ya kusema kwamba nilimuita chumbani, kwamba nimemwambia amtoe mama yake mzazi inahuzunisha.

"Sina namna,mtoto akiunyea mkono huwezi kuukata, nimemuachia Mungu,nimemsamehe na ninamuombea, sihitaji msamaha wowote kutoka kwake akiona kuna tija sawa.

"Akiona kuna haja ya kuomba msamaha watu waliosikia maneno hayo ni sawa,lakini anayestahili kuombwa msamaha zaidi ni Mwenyenzi Mungu,”amesisitiza Harmonize.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news