ARUSHA-Serikali kupitia Shirika la Nyumbu imeonesha dhamira ya kukifufua na kukiendeleza kiwanda cha kutengeneza magurudumu (matairi) kilichopo jijini Arusha cha General Tyre East Africa (GTEA) kilichoanzishwa miaka zaidi ya 50 iliyopita.
Shirika la Nyumbu (Tanzania Automotive Technology Centre-TATC Nyumbu) lilianzishwa kama Mradi wa Nyumbu mwaka 1977 ambao ulitokana na maono ya Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Desemba 14, 1985 Mradi wa Nyumbu ulibadilishwa na kuwa Shirika la TATC, ambalo lilianzishwa rasmi kwa Amri ya Rais chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Namba 17 ya mwaka 1969. Shirika liliwekwa chini ya Wizara ya Ulinzi na JKT.
Lengo kuu lilikuwa ni kuendeleza mapinduzi ya teknolojia za magari na mitambo nchini (Automotive Engineering) kwa kufanya utafiti na ubunifu ili Taifa liweze kujitegemea kiteknolojia.
Hayo yamebainika katika ziara maalum iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na uongozi wa shirika hilo katika eneo la kiwanda jijini humo ambayo ilikuwa mahususi katika kufanya tathmini.
RC Makonda amesema,wanataka kuona namna gani wanaweza kufufua kiwanda hicho ambacho ni tumaini kwa wananchi wa Arusha.
"Lengo letu ni kuhakikisha viwanda kama General Tyre vinafufuliwa kwa ushirikiano wa karibu na taasisi za umma na binafsi.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumbu, Balozi Luteni Jenerali mstaafu Yusuph Kisamba alisema kuwa,hatua za awali zimeanza kuchukuliwa ili kuwekeza katika kiwanda hicho kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara.
Amesema,shirika linaangalia uwezekano wa kuwekeza katika kiwanda hicho kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara.
"Tayari tumeshafanya tathmini ya awali ya miundombinu na mahitaji muhimu kwa ajili ya uendelezaji wa kiwanda.”
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumbu, Kanali Charles John Kalambo ameeleza kuwa, shirika lake liko tayari kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani:
Mshauri wa kiufundi wa Shirika la Nyumbu, Mhandisi Juma Kassim Kumbikila, alieleza kuwa mazingira ya kiwanda bado yako katika hali nzuri na yanaweza kutumika kwa upanuzi wa uzalishaji:
Pia, amesema eneo la ekari 50.4 lililokuwa likitumika na General Tyre bado lipo katika hali nzuri na linaweza kutumika kwa upanuzi wa uzalishaji.
Ikumbukwe kuwa, General Tyre ni kiwanda cha kutengeneza magurudumu Tanzania ambapo kilianza kujengwa mwaka 1969 na kuanza utengenezaji wa magurudumu mwaka 1971.
Kiwanda hiki kiliacha uzalizaji mwaka 2007 na kufungwa rasmi mwaka 2009 ambapo kwa nyakati tofauti Serikali imeonesha utayari wa kukifufua ili kiendelee na uzalishaji.
