Tanzania yazidi kung’ara kidijitali,AfIGF 2025 kufanyika Dar

NA GODFREY NNKO

TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Jukwaa la Afrika la Usimamizi wa Mtandao (14th Africa Internet Governance Forum-AfIGF) kwa mwaka 2025.
Hayo yamebainishwa leo Mei 22,2025 na Mkurugenzi wa Miundombinu ya TEHAMA wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Leo Magomba wakati akifungua semina kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelekea katika mkutano huo.

Amesema, mkutano huo ambao utaongozwa na kauli mbiu ya Kuwezesha Mustakabali wa Kidijitali wa Afrika utaanza Mei 29 hadi 31, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Jukwaa hilo la wazi litazileta pamoja Serikali na wabunge kutoka mataifa mbalimbali, mashirika mbalimbali na wadau kutoka sekta binafsi.

Vilevile jukwaa hilo litawaleta pamoja wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), wanazuoni, vijana, vyombo vya habari na wanafunzi.
Amesema,lengo la jukwaa hilo la kwanza kufanyika hapa nchini ni kujenga ushirikiano wa pamoja katika kuunda sera na mifumo ya kidijitali inayohudumia maslahi ya wote barani Afrika kwa ustawi bora wa huduma za intaneti.

Katika jukwaa hilo, wataalamu wa masuala ya mtandao barani Afrika watajadili kwa kina mada mbalimbali ikiwemo Akili Unde (AI) na teknolojia zinazoibuka,miundombinu ya umma ya kidijitali na usimamizi wa takwimu.

Mada nyingine amesema, ni kuhusu usalama wa mtandao,ustahimilivu na uaminifu wa kidijitali, upatikanaji na uunganishaji wa huduma za kidijitali na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kidigitali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news