Kuelekea Siku ya Fistula Duniani, wadau wa afya wakutana kujadili afua muhimu

MBEYA-Watoa huduma za Afya ya Mama na mtoto wametakiwa kuwa makini wakati wa utoaji huduma ya uzazi ili mama anapojifungua mtoto asibaki na changamoto yoyote ya kiafya ikiwemo kupata ugonjwa wa fistula.Rai hiyo imetolewa Mei 21, 2025 jijini Mbeya na Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Godlove Mbwaji kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kujadili afua muhimu kuhusu namna bora ya kupambana na ugonjwa wa Fistula kwa akina mama.

Dkt. Mbwanji amesema Serikali imewekeza katika huduma za mama na mtoto, hivyo ni wajibu wa watoa huduma kuhakikisha hatakiwi kupata tatizo lolote wakati wa kujifungua.
"Tunajua mama anapomleta mtoto duniani hatakiwi kuwa na tatizo lolote na wote tunajua ni muhimu sana huyu mama wa thamani kumlinda dhidi ya fistula ili kuwa na uzazi endelevu katika Taifa letu," amesema Dkt. Mbwanji.

Naye Mratibu wa Afua za Fistula Tanzania Bi. Fidea Obimbo amesema Wizara ya Afya inachukua hatua muhimu kupambana na ugonjwa wa Fistula kwa kutoa huduma karibu kwa wananchi akitaja huduma za kibingwa za madaktari wa Dkt. Samia kuwa sehemu ya mapambano hayo.

Bi. Fidea ameongeza kuwa maadhimisho hayo mwaka huu yanafanyika Mbeya katika hospitali Kitengo cha Huduma ya Mama na mtoto ili kuenzi wakina mama na kutoa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa wenye changamoto ya Fistula.
Bi. Fidea ametoa wito kwa wadau wa Afya kujitokeza kwa wingi kutoa michango yao katika mapambano dhidi ya Fistula akisema kuwa idadi ya wadau wanotoa huduma katika eneo la ugonjwa huo bado ni ndogo sana.

Naye Mkurugenzi wa Fistula Foundation Bw. Clement Ndahani akiongea na vyombo vya habari amesema ugonjwa wa fistula unawakumba wengi wanaotoka katika kaya masikini.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi Dkt. Rebeca Mokeha amesema mkoa wa Mbeya unakabiliwa kuwa na wagonjwa wa Fistula takribani 3000 lakini upasuaji unafanyika kwa wagonjwa 1000 pekee kwa sababu watu wengi hawajitokezi kutokana na imani potofu katika jamii kuwa fistula ni laana na baadhi huamini kuwa ugonjwa huo hautibiki.
Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Fistula Duniani uhadhimishwa kila mwaka na kwa mwaka 2025 yanafanyika Mkoani Mbeya yakiwa na kauli mbiu isemayo Afya ni Haki ya Kila Mwanamke, Tengeneza Hatma yake, Pasipo Fistula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news