NA MARY GWERA
Mahakama
MSAJILI Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya ameushukuru Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kukubali ombi la Mahakama hiyo kuja kujifunza na kusema kwamba wamepata maarifa ya kutosha yatakayowawezesha kutekeleza nchini mwao ili kuboresha huduma za utoaji haki kwa manufaa ya wananchi wa nchi hiyo.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya (wa tano kushoto) pamoja na sehemu ya wajumbe kutoka Mahakama hiyo na Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja ndani ya moja ya kumbi za Mahakama (court room) kwenye Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza leo tarehe 22 Mei, 2025 katika mahojiano maalum yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Mokaya amesema kuwa, wamepata mapokezi mazuri na kufurahia kila hatua ya ziara yao.
“Tumekamilisha ziara yetu leo, tulianza kwa kutembelea Kituo Jumuishi cha Mahakama Temeke tuliweza kuona jinsi Mahakama hiyo inavyofanya kazi, tuliona pia Mahakama Inayotembea inavyotoa huduma na vilevile tukaja Dodoma, tumefurahi tumepokelewa vizuri na Jaji Kiongozi, Msajili Mkuu na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania ambao tumekuwa nao muda wote, tunaahidi tutakeleza yote tuliyojifunza,” amesema Mhe. Mokaya.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya akiwa katika moja ya kumbi ya Mahakama iliyopo ndani ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma pindi yeye pamoja na ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya walipotembelea jengo hilo leo tarehe 22 Mei, 2025.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya pamoja na baadhi ya ujumbe wa watumishi kutoka Mahakama hiyo wakiwa ndani ya chumba maalum cha kunyonyeshea kilichopo ndani ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya (kushoto) pamoja na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo wakiwa ndani ya chumba cha watoto kilichopo ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania wakati ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya walipotembelea chumba hicho kilichopo ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya.
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya na sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania.
Amesema kuwa, yeye pamoja na timu yake wamefurahi kuona jinsi Mahakama ya Tanzania ilivyoboresha huduma zake na kuwa Mahakama ya wananchi yenye miundombinu inayozingatia mahitaji ya wananchi.
“Tumefurahi pia kuona maendeleo makubwa ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ndani ya Mahakama ya Tanzania pamoja na miundombinu mizuri ya majengo ambayo inaonesha kuzingatia na kuthamini utu wa watumishi wake pamoja na wananchi wanaohudumiwa,” ameeleza Msajili Mkuu huyo.
Ameongeza kuwa, Mahakama zote duniani zina changamoto zake, hivyo inahitaji uthubutu katika kufanya mageuzi ya kuboresha huduma na hilo limethibitishwa na Mahakama ya Tanzania na kwamba nao wamejifunza na kuahidi kufanyia kazi yote waliyojifunza.
Kadhalika, Mhe. Mokaya amewakaribisha pia Mahakama ya Tanzania kutembelea Mahakama ya Kenya kujifunza na kubadilishana uzoefu ili kuendelea kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya pamoja na Watumishi wengine kutoka Mahakama hiyo wakipanda miti ya kumbukumbu kwenye eneo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya ukiongozwa na Msajili Mkuu wa Mahakama hiyo, Mhe. Winifrida Mokaya wakiwa katika jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama walipotembelea Ofisi hiyo leo tarehe 22 Mei, 2025 ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha ziara yao ya kujifunza.
Aidha, ujumbe huo umekutana pia na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ambaye amezungumza nao na kusema nao kuwa, ili Mahakama iweze kufanikiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ni muhimu kushirikiana na mihimili yote ya Dola ikiwa ni Serikali na Bunge.
Katika Siku ya mwisho ya ziara yao , ujumbe huo umetembelea jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na kujionea chumba cha kunyonyeshea Watoto, chumba cha Watoto, ukumbi wa Mahakama (Court room). Vilevile wametembelea jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama lililopo Jirani na jengo la Mahakama.


