NA GODFREY NNKO
OFISI ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) inatarajia kuendesha mafunzo maalum kwa mawakili wote wa Serikali kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
Mafunzo hayo yatajumuisha mawakili kutoka wizara, taasisi zote za Serikali, mashirika, mamlaka za tawala za mikoa na Serikali za mitaa.
Aidha,mafunzo hayo yatafanyika kuanzia Juni 2 hadi 4,2025 katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Hayo yamesemwa leo Mei 28,2025 jijini Dar es Salaam na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt.Ally Possi wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake.
Amesema, kupitia mafunzo hayo mawakili wa Serikali watajifunza mbinu za kisasa na kupata uwezo wa ziada wa kufanya kazi kwa ufanisi na weledi zaidi ambapo Juni 3,2025 yatafunguliwa rasmi na Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt.Damas Ndumbaro.
Vilevile, amesema mafunzo hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo "Ubobezi wa Sheria kwa Ajili ya Kesho:Teknolojia, Mikakati na Mizania Binafsi kwa Mawakili wa Serikali katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050"
Dkt.Possi amesema, mafunzo hayo yamefanyika kwa miaka mitano mfululizo sasa tangu mwaka 2020 ambapo, pia mawakili watapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa.
Kuhusu OWMS
Dkt.Possi amesema,Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) ilianzishwa kupitia Amri ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania iliyotangazwa Februari 13,2018 katika Gazeti la Serikali Na. 50 la mwaka 2018.
Amri hiyo ilitolewa kwa Mamlaka aliyonayo Rais kwa mujibu wa Ibara ya 36 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 48 la Mwaka 2018.
Pamoja na mambo mengine, amesema yalifanyika marekebisho ya Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (Office of the Attorney General (Re-structure) Order, 2018. (GN.No. 48 of 2018) kuanzisha ofisi tatu ambazo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS).
Dkt.Possi amesema,lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ni kuwa na taasisi moja ya Serikali itakayowajibika na utoaji wa huduma za kisheria kwa Serikali na taasisi zake katika maeneo ya uratibu, usimamizi, ushauri na uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake ndani na nje ya nchi.
Pia, kuingilia kati na kuendesha mashauri ya taasisi binafsi pale ambapo mashauri husika yana maslahi ya umma au yanahusu mali ya umma.
Tags
Breaking News
Habari
Mawakili Tanzania
Mawakili wa Serikali
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
Wakili Mkuu wa Serikali
