NA DR MOHAMED MAGUO
MEI 5,2025 wanafunzi wa Kidato cha Sita kote nchini wataanza kufanya mitihani yao ikiwa ni hatua muhimu ya kuhitimisha masomo ya miaka miwili ya elimu ya sekondari katika ngazi ya A-level.
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) ndilo lenye jukumu la kusimamia na kuendesha zoezi la ufanyikaji wa mitihani hii.
Ikumbukwe mitihani ya Kidato cha Sita ni muhimu katika mtaala wa elimu nchini kwa sababu ndio mitihani ambayo hutumika kama kigezo cha wanafunzi kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.
Kwa msingi huo huu ni utenzi wa kuwatakia heri na baraka wanafunzi wote wa kidato cha sita wanapoelekea kuanza mitihani ya mwisho ya Taifa ya kuhitimu.
Tunawaomba walimu wawasomee au wawape wanafunzi waghani utenzi huu katika siku hizi chache zilizosalia kabla ya kuanza kwa mitihani hiyo. Endelea;
¹Salamu kwenu jamia
Cha sita cha Tanzania
Heri nyingi watakia
Mfaulu kwa kishindo
²Mitihani 'mewadia
Mwezi huu wa Meia
Sote twawaaminia
Mtafaulu viwango
³Ukipewa karatasi
Mtihani sipepesi
Jiraniyo kumghasi
Komaa na 'paper' lako
⁴Jitulize usiwasi
Tafakari kwa nafasi
Moyo wako na nafsi
Vitulie tulizana
⁵Kudesa eti kudesi
Ndugu yake kugesi
Utazikosa makisi
Uambulie papatupu
⁶Ukipewa karatasi
'Ndoa wako wasiwasi
Kokotoa kwa nafasi
Maswali uloulizwa
⁷'Sikimbie mwendo kasi
Uonapo ukakasi
Tafakari halasi
Majibu utayapata
⁸Vijana nyie makini
Na tena mwajiamini
Mtafuzu mitihani
Ufaulu wa kishindo
⁹Mliyofunzwa shuleni
'Mewajenga tamrini
Someni zingatieni
Mtafaulu viwango
¹⁰Sisi wana wahuria
Sala Dua wafanyia
Mwenyezi wasimamia
Mfaulu kwa kishindo
MTUNZI
Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mshairi wa Kisasa
Mhadhiri Mwandamizi
Mkuu wa Itifaki
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
