Profesa Kabudi aishauri Afrika kuzingatia mambo haya

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema,ili Bara la Afrika liweze kupaa zaidi katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiuchumi viongozi wa mataifa yote wanapaswa kuzingatia mambo muhimu.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuwa na juhudi za pamoja katika kujenga mataifa imara yenye maendeleo endelevu na uwezo wa kutoa huduma bora kwa raia wake (states development).

Ameyasema hayo leo Mei 24,2025 katika Mhadhara wa 15 wa Siku ya Afrika ya Thabo Mbeki (The Thabo Mbeki 15th Africa Day Lecture) uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Pia, amesema juhudi hizo zinapaswa kujikita katika kuboresha na kuimarisha taasisi, uchumi, miundombinu, utawala, sheria, elimu, afya na sekta nyingine muhimu katika kila taifa ili kuhakikisha ustawi wa wananchi na ufanisi wa serikali.

Jambo lingine,Mheshimiwa Profesa Kabudi amesema, wananchi wanapaswa kushirikishwa katika kila hatua za maendeleo ili waweze kushiriki kikamilifu kuhakikisha malengo yanafikiwa.

Amesema, ushiriki wao unaweza kuhusishwa kwa namna mbalimbali ikiwemo mawazo, ujuzi,ubunifu na namna nyinginezo.

Vilevile amesema, kutokana na rasilimali zilizopo katika bahari, maziwa na mito, Afrika inapaswa kuwekeza ujuzi wa kutosha kwa watu wake ili waweze kuzisimamia na kuzivuna rasilimali hizo kwa utaratibu ambao utakuwa na manufaa makubwa katika uchumi kwa jamii na bara lote kwa ujumla (uchumi wa buluu).

Profesa Kabudi, pia amehimiza uwekezaji na matumizi ya teknolojia na rasilimali zinazohusiana na anga ya juu kwa madhumuni ya kibiashara na maendeleo ya uchumi barani Afrika.

Amesema, uwekezaji katika teknolojia kuna faida nyingi ambazo si tu kwamba zitaleta tija kwa bara hilo, bali pia itapanua wigo katika sekta nyingine za uzalishaji.

Katika hatua nyingine, Profesa Kabudi amesisitiza umuhimu wa Bara la Afrika kuwa na mageuzi chanya katika viwanda huku akishauri rasilimali zinazopatikana barani humo zinatosha kuzalisha bidhaa na kuhudumia masoko ya ndani na nje.

Amesema, Afrika imejaliwa rasilimali za asili ambazo zina upekee yakiwemo madini adimu ambapo zikitumika na kusimamiwa vizuri uchumi wa bara hilo utaimarika zaidi.

Waziri Profesa Kabudi amesema, pia Afrika inapaswa kuwekeza vya kutosha katika elimu na usafiri wa anga, kwani sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi kupitia usafirishaji.

Mambo mengine, Profesa Kabudi amesema, Afrika inapaswa kutumia rasilimali zake katika kubuni na kuendeleza nishati ikiwemo nishati safi kwa matumizi mbalimbali.

Aidha, amehimiza umuhimu wa Afrika kuwa na mkakati wa pamoja wa kuhakikisha wanazalisha vifaa tiba na dawa ili kuepuka gharama kubwa ambazo huwa zinatumika kuagiza kutoka nje ya bara hilo.

Profesa Kabudi ametolea mfano kuwa, wakati UVIKO-19 ilivyopampa moto, kuna baadhi ya Waafrika walikuja na bunifu zao ikiwemo vitakasa mikono na barakoa ambazo zilionesha mafanikio mazuri.

Amesema, bunifu za namna hiyo zinapaswa kuungwa mkono ili kuhakikisha Waafrika wenyewe wanatimiza malengo yao bila utegemezi.

Wakati huo huo, Profesa Kabudi amesema, Afrika ili iweze kufikia malengo yake inapaswa kujiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa miradi au mipango inatekelezwa kwa ufanisi, kwa kutumia usimamizi wa karibu, ukaguzi wa mara kwa mara na uchambuzi wa matokeo ili kufahamu hatua inayoendelea inaanzia wapi.

Mhadhara wa Siku ya Afrika ya Thabo Mbeki ni tukio la kila mwaka linaloandaliwa na Thabo Mbeki Foundation (TMF) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (Unisa) kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Afrika.

Ni siku ambayo huadhimisha kuanzishwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU) Mei 25, 1963, huko Addis Ababa, Ethiopia.

Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 62 tangu kuanzishwa kwa OAU, ambayo ndiyo chimbuko la Umoja wa Afrika (AU) uliozinduliwa rasmi huko Durban, Afrika Kusini mwaka 2002.

Uamuzi wa kuandaa Mhadhara wa 15 wa Siku ya Afrika ya Thabo Mbeki nchini Tanzania mwaka huu unatokana na mchango mkubwa wa Tanzania katika historia ya Bara la Afrika ukiwa umejengwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wakfu wa Thabo Mbeki kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo walikuwa wenyeji wa mhadhara huo wa kila mwaka wa Siku ya Afrika.

Mhadhara huo umewaleta pamoja viongozi na wadau kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika ili kutafakari maendeleo ya bara na mustakabali wake kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news