NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amempongeza, Prof. Mohamed Yakub Janabi, kwa kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika kuanzia sasa hadi mwaka 2030.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa pongezi hizo kupitia mitandao yake ya kijamii muda mfupi baada ya Profesa Janabi kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo.
Katika kikao maalum cha pili kilichoketi leo Mei 18, 2025 jijini Geneva nchini Uswisi. Profesa Janabi ameshinda kwa kura 32 kati ya kura 46 ambapo alikuwa akichuana na N’da Konan Michel kutoka Ivory Coast.
Mohammed Lamine kutoka Guinea, Dkt. Boureima Hama Sambo kutoka Niger, Profesa Moustafa Mijiyawa kutoka Jamhuri ya Togo.
Profesa Janabi ameshinda nafasi hiyo iliyoiachwa wazi na aliyekuwa Mkurugenzi Mteule, Dkt.Faustine Ndugulile ambaye alifariki Novemba 27, 2024.
"Hongera kwa Profesa Mohamed Yakub Janabi kwa kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2030.
"Kwa uzoefu na ujuzi wa miongo kadhaa katika sekta ya afya, nina imani kubwa kwamba una kila sifa na uwezo wa kuutumikia bara letu na kutuongoza kufikia mafanikio makubwa zaidi.
"Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa shukrani kwa kila nchi mwanachama iliyotambua uwezo, uzoefu na maono yako kwa ajili ya bara letu.
Profesa, nakutakia kila la heri katika kipindi chako cha uongozi."
Katika hatua nyingine,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus amempongeza Profesa Mohamed Yakub Janabi kwa ushindi huo.
"Ninaamini ataiongoza Kanda ya Afrika kwa ufanisi mkubwa na kuleta mabadiliko chanya katika mifumo ya afya barani humo," amesema Dkt. Tedros.
Mkurugenzi Mkuu huyo ameongeza kuwa, WHO iko tayari kumpa ushirikiano wa karibu katika kutekeleza majukumu yake mapya.
Aidha,amesitiza kuwa,uteuzi wake ni ushahidi wa kuaminiwa kwake kimataifa na mchango wake katika afya ya jamii.
Kuhusu WHO
Shirika la Afya Duniani (WHO) ni wakala maalumu wa Umoja wa Mataifa unaohusika na afya ya umma ya kimataifa. Jukumu rasmi la WHO ni kukuza afya na usalama huku kusaidia walio hatarini kote ulimwenguni.
Hutoa usaidizi wa kiufundi kwa nchi, huweka viwango vya afya vya kimataifa, hukusanya data kuhusu masuala ya afya duniani, na hutumika kama jukwaa la majadiliano ya kisayansi au sera kuhusiana na afya.
