ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amempongeza Profesa Mohamed Yakoub Janabi kwa kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi kupitia pongezi zake hizo ameeleza kuwa,uteuzi huu ni uthibitisho wa mchango mkubwa alioutoa Profesa Janabi katika sekta ya afya, pamoja na dhamira yake ya kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika.
"Zanzibar itaendelea kuunga mkono ajenda ya afya ya kikanda na kimataifa, pamoja na kushirikiana kwa karibu na Profesa Janabi katika juhudi za pamoja za kuboresha huduma za afya."
Katika kikao maalum cha pili kilichoketi leo Mei 18, 2025 jijini Geneva nchini Uswisi. Profesa Janabi ameshinda kwa kura 32 kati ya kura 46 ambapo alikuwa akichuana na N’da Konan Michel kutoka Ivory Coast.
Mohammed Lamine kutoka Guinea, Dkt. Boureima Hama Sambo kutoka Niger, Profesa Moustafa Mijiyawa kutoka Jamhuri ya Togo.
Profesa Janabi ameshinda nafasi hiyo iliyoiachwa wazi na aliyekuwa Mkurugenzi Mteule, Dkt.Faustine Ndugulile ambaye alifariki Novemba 27, 2024.
