NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan amezindua Sera mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 toleo la mwaka 2024 huku akisisitiza kwamba hatatoa nafasi Kwa kiumbe chochote kuvuruga nchi yetu.
Akizindua sera hiyo jijini Dar es Salaam leo Mei 19,2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), pia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini kutotoa nafasi kwa watovu wa nidhamu toka nje ya nchi kutuvuruga.
"Tusiwe shamba la Bibi kwamba mtu anaweza kuja Tanzania akasema analolitaka, lipo Tanzania halipo, watu wakajisemea tu, tumeanza kuona mwenendo wa wanaharakati ndani ya ukanda huu kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku.
"Sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia, tusitoe nafasi walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika ni hapa kwetu, niwaombe vyombo vya ulinzi na usalama kutotoa nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kutovuka hapa kwetu, hapana.
“Nimeona clip kadhaa za kunisema, nipo bias na nini, ninalofanya ni kulinda nchi yangu na ndiyo wajibu wangu niliopewa, kwa hiyo hatutotoa nafasi kwa kiumbe yeyote kuja kutuvurugia hapa awe yupo ndani ama anayetoka nje.”
Amesema kuwa, ili kulinda uhuru na heshima ya nchi tusikubali watu kumtumia teknolojia kufanya wanachotaka na kuitaka wizara kuchukua hatua za haraka ili nchi isiwe shamba la bibi kila mtu kusema anachotaka.
Katika hatua nyingine Rais Dkt. Samia alitoa maelekezo kwa wizara mahususi kuhakikisha utoaji wa mafunzo kuhusu mantiki ya sera kwa watumishi wa umma na kwamba wanaweza kuwatumia mabalozi wastaafu kuelezea sera hiyo kwa sekta mbalimbali.
Pia amewataka mabalozi wa Tanzania nje ya nchi waisome na kuilewa vizuri sera hiyo kwa lengo la kuitangaza kikamilifu na pia Wizara, Idara na Taasisi kuhakikisha wanajumuisha malengo ya sera.
Dkt.Samia amesema, kwa kuwa watanzania waishio nje ya nchi Diaspora wametambuliwa kama wadau muhimu wa maendeleo waje kuwekeza nyumbani na sio kuisema vibaya nchi yao na kuzitaka sekta binafsi toka nje zifanye uwekezaji hapa nchini.
Amesema kuwa,uhusiano na diplomasia ya Kimataifa ni suala linalohusu pia ulinzi na usalama wa nchi hivyo ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama nchini Tanzania kuhakikisha kuwa wanajidhatiti katika kudhibiti vitendo vya uhalifu wa kuvuka mipaka.
Sambamba na matendo ya kigaidi yanayoendelea kote duniani kwa kuhakikisha mipaka inakuwa salama na amani inatamalaki kote Tanzania.
Vilevile amewataka wananchi na sekta binafsi nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii zilizopo nchini.
Rais Dkt.Samia amezitaka mamlaka zinazosimamia ajira nje ya nchi kuja na sera na sheria rafiki kwa Watanzania ili waweze kufaidika na mahusiano mema ya Tanzania na mataifa mengine kote duniani ambayo yamekuwa yakitoa fursa za ajira kwa raia wa kigeni.
Aidha,sera hiyo ni zao la maboresho ya Sera ya mwaka 2001 (Toleo la 2024 la Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001.
Rais Dkt.Samia ameshiriki katika tukio hilo muhimu ambalo linaangazia mwelekeo mpya wa Diplomasia ya Tanzania katika karne ya 21.
Naye, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amesema sera hiyo ni kielelezo cha taifa kukua kwa vitendo, demokrasia ya uchumi na uchumi wa bluu.
Aidha, amesema kuwa Sera hiyo inalenga kufungua milango ya fursa mpya za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa pande zote za Muungano, hususan Zanzibar, ambayo kwa kiwango kikubwa inategemea sekta ya nje kwa maendeleo yake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 19 Mei, 2025. Kushoto kwake ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema, Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 imefanyiwa marekebisho ili kuendana na mabadiliko mbalimbali duniani ambapo pia, wadau mbalimbali walishiriki kutoa maoni na mapendekezo.
Sera mpya imejumuisha mambo kadhaa ikiwemo kulinda maslahi ya taifa kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa kuzingatia misingi ya uhuru,haki za binadamu, demokrasia na ujirani mwema.
Vilevile, imelenga kukuza diplomasia ya uchumi, kulinda maslahi ya taifa, kuendeleza uhusiano na nchi na taasisi mbalimbali na kuchangia maendeleo duniani.
Balozi Kombo pia alibainisha kuwa,sera mpya imelenga kujenga mazingira wezeshi ya ndani, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
Pia kushughulikia masuala ya madeni, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa na kudumisha misingi ya sera ya kutofungamana na upande wowote duniani.
Amesema sera hiyo imekuja katika kipindi ambacho, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anaendelea kusalia kuwa shujaa zaidi kwa kuimarisha Diplomasia ya Tanzania kote Duniani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo la Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kabla ya uzinduzi wa Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 19 Mei, 2025.
Ikumbukwe, tangu Mheshimiwa Rais Dkt.Samia aingie madarakani mwaka 2021 amefanikiwa kurejesha uhusiano wa kimataifa, kuvutia uwekezaji, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Jitihada hizo zimesaidia kuboresha uchumi, kuongeza nafasi ya Tanzania kimataifa na kukuza amani na usalama ndani na nje ya nchi.