Rushwa ya shilingi 210,000 yamponza Mtendaji wa Kata

KIGOMA-Mtendaji wa Kata ya Rungwe Mpya iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma,Bi.Tausi Issa Manyanya amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Shauri lake limefunguliwa Mei 15,2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Kasulu. Aidha,shauri hilo la jinai CC 11711/2025 limefunguliwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kasulu,Mheshimiwa Emaculate Emanuel Shulli (RM), kati ya Jamhuri dhidi ya Afisa Mtendaji huyo.

Mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili kwa kuvunja kifungu cha 15(1) (a) na 15(2) kinachohusu kushawishi na kupokea hongo kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya 2022.

Ilidaiwa kwamba, Bi. Tausi Issa Manyanya, akiwa katika Kijiji cha Rungwe Mpya Kata ya Rungwe Mpya Halmashauri ya Wilaya Kasulu, aliomba na kupokea hongo kiasi cha Tsh. 210,000.

Ni kutoka kwa Bw. Omari Haruna ambaye ni mfugaji na mkazi wa Kijiji cha Kigembe ili aweze kuruhusu mfugaji huyo aweze kupatiwa ng'ombe wake mmoja aliyekuwa amepotea na kupatikana katika Kijiji cha Rungwe Mpya.

Ng'ombe huyo alihifadhiwa kwa mfugaji Longo Lugata Shija wa kitongoji cha Osterbey kilichopo Kijiji cha Rungwe Mpya kwa maelekezo ya Bi. Tausi Issa Manyanya Afisa Mtendaji Kata ya Rungwe Mpya.

Aidha,mshtakiwa huyo alikana mashtaka yote katika shauri hilo aliyosomewa na Waendesha Mashtaka wa Serikali kutoka TAKUKURU Bw. James Mosi Nyarobi na Bw. Davis Jason Junior

Mshitakiwa aliachiliwa baada ya kukidhi masharti ya dhamana ya Mahakama na shauri hilo litaendelea tena mahakamani hapo Juni 2,2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news