DODOMA-Mbunge wa Singida Mashariki na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu ameipongeza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Tume ya TEHAMA nchini (ICTC) kwa kuanzisha vituo vya ubunifu kwa ajili ya mbunifu yeyote bila kujali ana elimu au hana elimu nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt.Nkundwe Mwasaga akitoa majina ya washindi tayari kwa kutangazwa katika TEHAMA Awards hivi karibuni jijini Arusha. Kazi ya kuchuja na mchakato wote ulifanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Deloitte. (Picha zote na Maktaba ya Tume ya TEHAMA).
Sambamba na kuja na Tuzo za TEHAMA 2025 (TEHAMA Awards) ambazo zimefanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu wa 2025 jijini Arusha huku zikiibua hamasa kubwa ya ushindani kwa vijana nchini.
Ametoa pongezi hizo leo Mei 16,2025 wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya shilingi bilioni 291.5 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa wizara hiyo,Mheshimiwa Jerry Silaa.
"Na nikupongeze sana,tulipokuwa pale Arusha (mwaka huu 2025) mliweza hata kutoa tuzo kwa vijana wabunifu wa Tanzania."
Mheshimiwa Mtaturu amesema, tukio hilo lilikuwa la faraja zaidi,kwani vijana wengine walitokwa na machozi ya furaha kwa kuwa hawakutarajia kupata tuzo ya namna hiyo.
"Mheshimiwa Waziri jambo lile endelea nalo. Endelea nalo kwenye mikoa yote isiwe eneo moja Dar es Salaam na Arusha, nenda mikoa yote Tanzania, vijana wabunifu wapo na tuwajengee uwezo kuwatia moyo."
Vilevile amesema, alifurahishwa na namna ambavyo pia vijana hao walipatiwa mitaji.
"Yaani kijana ameanzisha ubunifu wake, hana uwezo wa fedha, mnampa fedha ili aweze kukuza ubunifu wake aweze kuajiri vijana wengine."
Amesema kuwa, hatua hiyo itapunguza changamoto ya vijana kubaki kwenye mambo ya michezo ya kubashiri na mambo mengine ambayo hayana tija.
Pia amesema, vijana wengi wa Kitanzania wana uwezo mkubwa katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hivyo kuwajengea uwezo ni kuwapa uhakika wa kukuza vipaji vyao.
Nafidh Ally Mola ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kozi ya Sayansi ya Kompyuta katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam akitokwa na machozi ya furaha baada ya kushinda tuzo hizo.
"Mheshimiwa Waziri uendelee kuwalea ili kuhakikisha vijana wetu wanapa fursa hii,ambayo kimsingi Rais amesema wizara yako ikisimamiwa vizuri itasaidia sana kuleta ajira nyingi kama ambavyo tumesema."
Pia, amesema vituo vya ubunifu viongezewe kasi ili viweze kukamilika ili vijana waanze kupata mafunzo.
"Lakini, si vijana tu,hata watu ambao wana shughuli zao nyingine wanaweza kwenda kujifunza pale na kuweza kupata uwezo mzuri zaidi wa kutumia TEHAMA."
Awali, alisema Sekta ya Mawasiliano ina mchango mkubwa nchini kwani ni kichocheo kikubwa cha ukuaji uchumi katika sekta nyingine.
"Mfano watu wa fedha,kwenye mambo ya miamala wanategemea sana wizara hii, mawasiliano ya simu yanategemea sana wizara hii, lakini pia ajira nyingi zitatokana na wizara hii ambayo inawagusa zaidi vijana wetu."
Kuhusu mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambao umefikia asilimia zaidi ya 70 kwa maana ya utekelezaji wake amesema kuwa,mradi huo una umuhimu mkubwa kwa Taifa.
Pia, ameeleza kuwa, Wizara iendelee kuusimamia mradi huo ili kuhakikisha mifumo ya taasisi inasomana kikamilifu.
"Tumesikia taasisi zaidi ya 100 kwa maana ya Bara na Visiwani wote kwa maana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeshafikiwa na mradi huu na zimeshaanza kusomana."
Amesema, ufanisi wa mradi huo si tu kwamba unakwenda kusaidia kuharakisha shughuli za maendeleo nchini, pia utaendelea kuipa Tanzania heshima kubwa duniani.
"Lakini, utasaidia sana kupunguza watu kulipa fedha taslimu.Watu watakuwa hawatumii fedha taslimu maeneo mbalimbali na itasaidia kwenye ukusanyaji wa kodi."
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt.Nkundwe Mwasaga amesema kuwa, miongoni mwa vituo hivyo vitakuwa mahususi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa za TEHAMA na vingine kwa ajili ya kukuza bunifu.
Katika vituo vya kutengeneza bidhaa, Dkt.Mwasaga alisema, kimoja kipo TIRDO na kingine SIDO jijini Arusha.
Pia, alisema kwa upande wa makao makuu ya Tume ya TEHAMA yaliyopo Upanga jijini Dar es Salaam kuna vituo viwili.
Kati ya vituo hivyo, Dkt.Mwasaga amesema kimoja ni kwa ajili ya kukuza bunifu za vijana na kuna kituo kingine ambacho ni kati ya vituo 17 vya Umoja wa Mawasiliano Duniani.
Aidha, alisema kituo kingine kipo mkoani Lindi, Zanzibar, Tanga, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Arusha viwili na Dar es Salaam vitatu vyote vikiwa ni kwa ajili ya vijana na Watanzania kwa ujumla.
Tags
Bunge la Bajeti
Habari
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Sekta ya TEHAMA Tanzania
Tume ya TEHAMA