NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa,thamani ya Shilingi ya Tanzania imeendelea kuimarika huku ukwasi wa fedha za kigeni katika soko ukiongezeka kutoka dola za Kimarekani milioni 40 hadi 70 kwa siku.
Mafanikio hayo yanakuja ikiwa ni siku chache zimepita tangu,Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za mwaka 2025 zianze kutumika nchini.
Hayo yamesemwa leo Mei 20,2025 na Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania,Emmanuel Julian Akaro katika semina kwa waandishi wa habari za uchumi na masoko ya fedha iliyofanyika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam.
Amesema, Machi 28,2025 Serikali kupitia Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwingulu Nchemba ilitoa kanuni ambazo zinahusiana na katazo na matumizi ya fedha za kigeni ndani ya nchi yetu.
“Katika katazo hilo, wananchi hawaruhusiwi kufanya, kutumia fedha za kigeni (sarafu ya kigeni) katika kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma ndani ya nchi.”
Amesema, katazo hilo linahusu kutangaza kwa bei,kuwezesha, kutoza ikiwemo kulazimisha kutumia fedha za kigeni kwenye kufanya miamala hapa nchini.
Vilevile, amesema kupitia kanuni hizo pia zimetoa miamala ambayo inaruhusiwa ambayo ipo ya aina nne. "Ya kwanza ni malipo ya Serikali kama mchango wake kwenye taasisi za Kimataifa ambazo zipo hapa nchini.Lakini,vilevile Balozi na mashirika ya Kimataifa yanaruhusiwa bado kupokea hizo huduma kwa kutumia sarafu za kigeni.
“Lakini, vilevile maduka ambayo hayatozi ushuru, bado yanaweza kutangaza bei zao na kutoza kwa sarafu za kigeni.
“Lakini, vilevile ukiacha maduka, kama ndugu mwananchi una mkopo ambao ni wa sarafu ya kigeni bado unaweza kuendelea kulipa, kurejesha mkopo huo kwa sababu ni eneo ambalo limeruhusiwa.
Akaro amesema, kuanzia Machi 28, 2025 mikataba yote ambayo inaingiwa ndani ya nchi inatakiwa iwe kwa shilingi ya Kitanzania.
“Mikataba ile ambayo ilikuwepo kabla ya hii sheria na kanuni kutolewa na Gazeti la Serikali Na.198 la Machi 28,2025 imeruhusiwa kuendelea na hii Serikali imeipa mwaka mmoja.
“Na hii ni muhimu ili wahusika wa pande zote mbili katika hii mikataba waweze kujadiliana na kuweza kubadilisha.”
Mkurugenzi huyo amesema kuwa, wamepewa mwaka mmoja kuweza kubadilisha.Amesema, pale ambapo inashindikana kufanya mabadiliko kwa sababu moja au nyingine kanuni zinataka wahusika waende Wizara ya Fedha ili kuomba kibali maalum kwa Waziri wa Fedha.
“Ni muhimu sana,ndugu wananchi kufahamu kwa kuwa na hizi kanuni umuhimu wake ni mkubwa katika kuhakikisha thamani ya shilingi yetu inaendelea kuimarika.”
“Tumeona ndani ya hiki kipindi kifupi ambacho hizi kanuni zimetoka,ukwasi kwenye soko la fedha za kigeni umeongezeka.
“Ukiangalia wastani wa kipindi cha mwezi mmoja, wastani wa siku, ukwasi wa dola kwenye soko la rejarereja umeongezeka kutoka dola milioni 40 hadi 67 mpaka 69 na hii ni kwa siku.Kwa hiyo,fedha nyingi za kigeni zimeingia sokoni.”
Amesema, chanzo cha ongezeko la ukwasi huo unatokana na wale ambao awali walikuwa wanatumia fedha za kigeni kufanya miamala ya moja kwa moja kwenda sokoni kwa ajili ya kubadilisha na kwenda kununua bidhaa au huduma eneo husika kwa shilingi ya Tanzania.
Amesema, hatua hii imeipa Serikali manufaa ya kuhakikisha shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa himilivu ukilinganisha na vipindi vya miaka ya nyuma kama sasa hivi.
“Tukumbuke soko letu la fedha za kigeni ni soko la msimu, ambalo kuanzia mwezi wa kwanza mpaka wa tano linakuwa ni soko ambalo lina mapato kidogo,fedha za kigeni zinakuwa zimepungua na kutoka hapo mapato ya fedha za kigeni yanakuwa yameongezeka sana.”
Amesema, kutokana na hali hiyo, shilingi ya Tanzania huwa inaendelea kuimarika zaidi, hivyo kwa mwaka huu fedha za kigeni zilizoko kwenye soko zimeongezeka.
“Ukilinganisha na mwaka jana kipindi kama hiki tulikuwa tuna dola milioni 30 kwa siku, sasa hivi tuna takribani dola milioni 69 mpaka 70 za Kimarekani kwa siku.”
Amesema, hayo ndiyo manufaa ambayo Serikali imeyapata ndani ya muda mfupi huku matarajio yakiwa makubwa zaidi mbeleni.
“Vilevile kwa kuhakikisha kwamba tunatumia shilingi, maana yake sasa, Sera za Benki Kuu ndizo zitakuwa zinatumika katika kuhakikisha mategemeo ya mfumuko wa bei yanasimamiwa vizuri na mfumuko wa bei unaendelea kuwa tulivu kwa asilimia 3.1.”
Pia, amesema kwa upande wa upatikanaji wa fedha za kigeni, Benki Kuu kama msimamizi wa Hazina ya Taifa ya Fedha za Kigeni wana hazina za kutosha.
Akaro amesema, wana zaidi ya akiba ambayo inaweza kulipia huduma na bidhaa kutoka nje miezi minne na nusu au zaidi.
“Lakini, vilevile tumekuwa kwenye mpango wa ununuzi wa dhahabu kuanzia mwaka jana mwezi wa 10 (2024). Huu mpango mpaka sasa hivi umetuongezea zaidi ya dola za kimarekani milioni 450 kwenye akiba yetu ya fedha za kigeni.”
Amesema, yote hayo yanalenga kuhakikisha Tanzania ina fedha za kigeni za kutosha.“Kwa hiyo, mtu ambaye pengine ana wasiwasi anataka alipwe dola leo ili aitumie baadae afahamu kwamba hizo fedha za kigeni zipo za kutosha."
Ameongeza kuwa, pale ambapo kutakuwa na mahitaji Benki Kuu ipo tayari kuweka fedha za kutosha sokoni.
Amesema, kwa mwaka huu pekee BoT imetoa zaidi ya dola milioni 130 kwenye soko ili kuhakikisha shilingi ya Tanzania inaendelea kuimarika.
Wakati huo huo, Akaro ametoa rai kwa kila anayehusika ikiwemo taasisi za kiserikali na binafsi kuhakikisha kwamba miamala yote ambayo inafanyika ndani ya nchi ifanyike kwa shilingi ya Tanzania na miamamla ambayo inafanyika nje ya nchi inafanyika kwa fedha za kigeni.
“Hii inafanya kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa nchi yetu, hii tunafanya kuhakikisha kwamba sarafu yetu inabaki imara.Sarafu imara maana yake ni uchumi imara, na ni maendeleo kwa kila mmoja wetu.”



