Gavana Tutuba aikaribisha Oman kuwekeza Tanzania

DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amelikaribisha Taifa la Oman kuendelea kuwekeza nchini hususan katika sekta ya fedha kutokana na mazingira rafiki ya kufanya biashara yaliyopo, na kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Tanzania.
Gavana Tutuba ameyasema hayo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud Al Shidhani, aliyeambatana na viongozi wakuu na waandamizi wa makampuni ya umma na binafsi kutoka Oman waliofika kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya fedha nchini.
Aidha, ameueleza ujumbe huo kuwa ripoti mbalimbali kutoka Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na taasisi za kimataifa zinazofanya tathmini ya mwenendo wa uchumi zinaonesha uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika.

Ameongeza kuwa sekta ya fedha ipo imara, ina mtaji na ukwasi wa kutosha, inajiendesha kwa faida na ubora wa rasilimali zake umeongezeka hali inayovutia zaidi uwekezaji katika sekta ya kibenki ili kuwafikia watanzania walio wengi zaidi.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Al Shidhani ameahidi kuendeleza ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu kati ya Oman na Tanzania kwa ajili ya kuchochea uwekezaji katika sekta ya fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news