DODOMA-Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana amesema,Tanzania imeendelea kuongoza Afrika na duniani kwa kuwa na simba wapatao 17,000 huku ikiongoza Afrika kwa wingi wa nyati.
Ameyasema hayo leo Mei 19,2025 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
"Nchi yetu Tanzania imeendelea kuongoza Afrika na duniani kwa kuwa na simba wapatao 17,000. Lakini, pia ikiongoza Afrika kwa nyati 225,000 na chui 24,000."
Vilevile,amesema takwimu zinaonesha kuwa idadi ya faru weusi imeongezeka kutoka faru 163 mwaka 2021 hadi 263 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 61.
Sambamba na hilo, Waziri Chana amesema, takwimu zinaonesha matukio ya ujangili wa tembo yamepungua kwa takribani asilimia 90.
Asali
Katika hatua nyingine Balozi Dkt.Pindi Chana amesema,hadi kufikia Aprili 2025, jumla ya tani 1,321.35 za asali zenye thamani ya shilingi 15,856,164,000.00 zimeuzwa nje ya nchi
sawa na asilimia 206.9 ikilinganishwa na kiasi cha tani 430.61 zenye thamani ya Shilingi 5,167,332,000.00 zilizouzwa nje ya nchi kwa kipindi kama hicho mwaka 2024.
"Kwa maendeleo haya, Shirika la Wafugaji Nyuki Duniani limeiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wafugaji nyuki duniani (APIMONDIA) mwaka 2027, utakaohudhuriwa na watu zaidi ya 4,000 kutoka sehemu mbalimbali za Dunia."
Ngorongoro
Pia,amesema neo la Hifadhi ya Ngorongoro limerejeshewa hadhi ya hifadhi ya jiolojia ya Ngorongoro Lengai (UNESCO Global Geopark).
"Mwaka 2022, eneo hili lilikua kwenye orodha ya hifadhi za jiolojia zilizopoteza hadhi, hata hivyo mwezi Desemba 2024 lilirejeshewa hadhi yake kutokana na juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita."
Miongoni mwa shughuli hizo,Waziri Chana amesema ni kuimarisha shughuli za uhifadhi katika maeneo ya urithi wa jiolojia,kutangaza pamoja na kufuata masharti na miongozo ya
UNESCO katika kulinda hadhi ya eneo hilo.
