DAR-Benki ya Biashara ya Tanzania (TCB) imejipanga kuendeleza mageuzi ya kidijitali ili kuongeza ujumuishi wa kifedha kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.
Katika upande wa ukuaji wa mizania ya kifedha,jumla ya mali za benki zimeongezeka kwa asilimia 25 hadi kufikia shilingi trilioni 1.74, na amana za wateja zimefikia shilingi trilioni 1.17 ikiwa ni ishara ya kuongezeka kwa imani ya wateja.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCB, Martin Emmenuel Kilimba katika mkutano mkuu wa 33 wa wanahisa.
Amesema, benki hiyo inaweka mkazo kwenye kuboresha miundombinu ya teknolojia ya kidijitali na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa makundi hayo muhimu ya uchumi, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya sekta binafsi na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 33 wa Wanahisa wa benki hiyo,Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Bw. Adam Mihayo amesema?TCB inalenga kuongeza ufanisi katika matumizi ya teknolojia mwaka huu wa fedha.
Vilevile kuendeleza suluhisho bora kwa wajasiriamali,kwani SMEs huchangia zaidi ya asilimia 95 ya biashara zote nchini na takribani asilimia 35 ya Pato la Taifa, hivyo kuwekeza katika huduma za kidijitali ni hatua muhimu ya kukuza sekta hiyo.
Bw. Mihayo amefafanua pia mafanikio ya kifedha yaliyopatikana mwaka 2024, ambapo benki ilipata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 44.81, kutoka kwenye hasara ya shilingi bilioni 44.42 mwaka 2023.















