DAR-Shirika la Reli Tanzania (TRC) limethibitisha kutokea kwa ajali ya treni ya mjini kwenda Pugu leo jioni majira ya saa 10:05, katika makutano ya reli na barabara ya Kawawa, ikiwa na mabehewa 12 yaliyojaa abiria takribani 1,200.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRC, ajali hiyo ilisababisha majeruhi 10 wakiwemo wanaume wawili na wanawake wanane ambao walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Amana kwa matibabu zaidi. Mabehewa sita kati ya 12 yalipata athari kutokana na ajali hiyo.Chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika na uchunguzi unaendelea. TRC imeahidi kutoa taarifa zaidi mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Huduma ya treni kati ya Stesheni ya Kamata na Pugu inatarajiwa kurejea kama kawaida kesho. TRC imetoa pole kwa wote walioathirika na ajali hiyo kwa namna moja au nyingine.
