Tuelekeze nguvu zetu kuziimarisha Madrassa, kuwasaidia masheikh na walimu-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza Waislamu, wahisani na wafadhili kuelekeza nguvu zao katika kuziimarisha Madrassa, kwani nyingi bado ziko katika mazingira yasiyoridhisha, pamoja na kuwasaidia Masheikh na Walimu wa Madrassa.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua Msikiti wa Jibril uliopo Fuoni Bwiti, Mkoa wa Mjini Magharibi, tarehe 16 Mei 2025.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali inafarijika inapowaona wadau na wafadhili mbalimbali wakijitokeza kusaidia huduma za kijamii katika sekta mbalimbali, kwani hatua hiyo husaidia kupunguza mzigo kwa Serikali.
Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza wana-Diaspora, hususan vijana wenye ujuzi katika ujenzi wa skuli, hospitali, huduma za afya na sekta nyingine za kijamii, kurejea nyumbani na kuungana na Serikali kuleta maendeleo ya taifa.

Akizungumzia Msikiti alioufunguwa, amewahimiza Waislamu kuutunza na kuutumia kwa ibada kwa bidii ili dhamira ya wafadhili waliochangia ujenzi wa msikiti huo itimie.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amezipongeza Taasisi za Tears of Joy na Jibril Foundation kwa usimamizi mzuri uliofanikisha ujenzi wa msikiti huo.
Kuhusu suala la amani, Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa Wazanzibari kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu ili nchi iendelee kupiga hatua zaidi za maendeleo.

Ameeleza kuwa mafanikio mengi yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yametokana na kuwepo kwa amani, jambo linalopaswa kuendelezwa kwani Serikali imejipanga kufanya mambo makubwa zaidi katika miaka mitano ijayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news