DAR-Tume ya TEHAMA (ICTC) imeshiriki kikamilifu katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka huu ambazo kwa Jiji la Dar es Salaam, ziliongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila.


Akizungumza baada ya sherehe hizo, Mkuu wa Kitengo cha Utawala na Rasilimali-Watu wa Tume ya TEHAMA, Bi. Flora Salakana, alisema ushiriki wa Tume katika maadhimisho hayo ni ishara ya kuthamini mchango wa rasilimali watu katika kukuza sekta ya TEHAMA na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Watumishi wetu ndio nguzo kuu ya utekelezaji wa majukumu ya Tume. Tunathamini sana kazi yao na tunaendelea kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza ufanisi,” alisema Bi. Salakana.
Kaulimbiu ya mwaka huu, "Uchaguzi Mkuu 2025 utuletee Viongozi wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi," imeakisi dhamira ya kutaka kuimarishwa kwa ustawi wa wafanyakazi ikiwemo kwenye sekta ya TEHAMA ambayo ni kiini cha uchumi wa kidijitali.