Tutumie intaneti kwa maendeleo,si kuumizana-Mhandisi Mahundi

NA GODFREY NNKO

NAIBU Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameitaka jamii na vijana kutumia intaneti katika misingi sahihi ili kujiletea maendeleo na si kuitumia kuumizana au kusambaza taarifa zenye kuleta taharuki na chuki.
Mhandisi Mahundi ameyasema hayo leo Mei 29,2025 wakati wa ufunguzi wa awali wa mjadala wa Kikao cha Mabunge ya Kikanda katika Mkutano wa 14 wa Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti Afrika (AfIGF) 2025 unaoendelea ndani ya kumbi za mikutano za Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Pia, Mheshimiwa Mahundi ameshiriki katika mkutano mwingine wa vijana ambao ni sehemu ya AfIGF ambapo amesema, "Vijana ndiyo watumiaji wakubwa wa intaneti na wao ndio wanaoshinda zaidi mitandaoni.

"Kwa hiyo, msipowashirikisha, wao watakuwa wanawaza mambo yao na ninyi huku viongozi mnawaza mambo yenu.
"Mwisho wa siku mnakuja kugongana, na mwisho wa siku badala ya vijana kuwa na matumizi sahihi kwa ajili labda ya kujifunza, kujielimisha, kuburudika, lakini vilevile kujiongezea maarifa sehemu mbalimbali na namna gani ya kushirikiana na nchi mbalimbali wakaenda sasa kushinda kwenye mitandao wakatumika vibaya na kuleta taswira ambayo siyo sahihi.

"Na wakati mwingine kusababisha hali ya kuitilafiana ambayo haifai katika jamii. Vijana ndio ambao tunawalea sasa, wafahamu mila, desturi na tamaduni zetu.

"Kwa hiyo, hata wakienda huko kwenye mitandao kwa sababu haina mipaka. Kijana akishaingia kwenye intaneti hakuna mpaka, kwa hiyo ni sisi kutoa elimu kwa vijana wetu kuhakikisha wanatumia vizuri hii mitandao, wasifanye vitu ambavyo havifai na wasitumike vibaya.

"Vilevile,kuwaongezea uzalendo waweze kuilinda nchi, kuiongea vizuri nchi kwa sababu au kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa.Kwa sababu, kupitia mitandao uchumi pia unakuwa kwa kasi."
Naibu Waziri huyo amesema,hivi ni vikao vya utangulizi kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano huo mkubwa ambapo mgeni rasmi Mei 30,2025 anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Dkt.Dotto Biteko.

Mkutano huo ambao mwenyeji ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unasimamiwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Amesema, katika mkutano huo masuala ya intaneti barani Afrika yatajadiliwa kwa mapana yake na mwishoni washiriki watatoka na mapendekezo mbalimbali ili kufahamu walipotoka,walipo na wanakoelekea kwa mustakabali mwema wa intaneti kwa kila nchi na Bara la Afrika kwa ujumla.

Pia, amesema dhamira ni kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa mpana kuhusu masuala ya intaneti.

Katika majadiliano ya mkutano huo, wamezunguzua zaidi namna ambavyo wanawake wamekuwa wakidhalilishwa hususani nyakati za uchaguzi.
Katika majadiliano hayo baina ya wabunge 40 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika wameweza kuelezana kwa undani changamoto ambazo zinaambatana na matumizi mabaya ya intaneti.

Aidha,majadiliano hayo yameangazia namna ambavyo wanasiasa wamekuwa wakikabiliwa na vikwazo vingi kwenye matumizi hasi ya taarifa, faida na hasara za matumizi ya intaneti katika kipindi hiki cha sayansi ba teknolojia.

Wakati huo huo,Mheshimiwa Mahundi amewaeleza washiriki wa mikutano hiyo upande wa vijana namna ambavyo Serikali kupitia wizara hiyo inatekeleza mipango thabiti ili kuhakikisha wananufaika kupitia bunifu na intaneti.

"Kama mnavyofahamu ndani ya wizara yetu tunaendeleza vijana, tunaibua vipaji na tunaruhusu hata watoto wa shule za msingi na sekondari kuonesha vipaji vyao."

Amesema, kwa nyakati tofauti taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo ikiwemo Tume ya TEHAMA na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zimekuwa zikiratibu mashindano mbalimbali ikiwemo ICT in Girls.

"Lakini, tulienda mbali zaidi tunajenga vituo vya kukuza bunifu, kwa hiyo vinaendekezwa na Tume ya TEHAMA nchini na tayari kwa sasa tuna vituo takribani nane katika mikoa mbalimbali."

Amesema, wanavyoshirikisha vijana ni kwa sababu wanaamini ndiyo watumiaji wakubwa wa intaneti na ndio wanaoshinda zaidi mitandaoni.
Mbali na hayo ametoa angalizo kwa wenye nia ovu kupitia intaneti katika uchaguzi ujao ambapo amesema,"Sisi kama Serikali tupo imara kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, TCRA, lakini kama wizara imejipanga vizuri, tutadhibiti wale wote ambao wanatumia vibaya mitandao, sheria itafuata mkondo wake.

"Hivyo, ninawasihi hata ili kundi la vijana ambalo nimetoka kuongea nalo hapo, waweze kutumika vizuri kwani tuna mambo mazuri sana ambayo yamefanywa na viongozi wetu, lakini vilevile hata na wagombea ambao nao wanatarajia kuwa viongozi kesho."

AfIGF 2025

Mkutano wa 14 wa Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti barani Afrika (AfIGF) unafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia leo Mei 29 hadi 31,2025 ukiongozwa na kaulimbiu ya 'Kuwezesha Mustakabali wa Kidijitali barani Afrika'.

Kupitia jukwaa hilo wadau wa masuala ya mtandao kutoka katika kanda mbalimbali na duniani kote wanakutana kujadili mustakabali wa dijitali wa Bara la Afrika.

Washiriki wanatoka serikalini,asasi za kiraia,sekta binafsi,jumuiya mbalimbali, taasisi za elimu ya juu na kwingineko.

Aidha,jukwaa hili ni sehemu ya majadiliano, ushirikiano na kubadilishana mawazo kuhusu masuala muhimu ya utawala wa mtandao barani Afrika,ukiangazia Miundombinu ya Umma ya Kidijitali na Usimamizi wa Taarifa, Akili Unde (AI) na Teknolojia Zinazochipukia.

Vilevile Usalama wa Mtandao, Uhimilivu, na Uaminifu,Upatikanaji wa Mtandao kwa Wote na Kuboresha Ushirikiano wa Kidijitali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news