NA JUMA MAULID
Bunda
WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Kata na Matawi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Jimbo la Bunda Vijijini, Wilaya ya Bunda mkoani Mara, wametishia kuandamana kwa madai ya kutokuwa na imani na Katibu wa chama hicho Wilaya ya Bunda, Michael Chonya, wakidai kuwa anashirikiana na Makatibu Kata kuondoa majina yao kwenye daftari la wajumbe watakapiga kura za maoni wakati wa uchaguzi ndani ya chama mwaka huu.
Wamesema watafikia hatua hiyo kama Chama hakitachukua hatua za haraka kurekebisha kasoro zilizopo, baada ya Makatibu Kata na Matawi kubadilisha majina ya wajumbe halali waliopitishwa na Chama mwaka 2022 na kuingiza majina yao binafsi wanayotaka wakifanya hivyo kwa maelekezo ya Katibu wa Wilaya ukiwa ni mpango mahsusi wa kulinda kura za Mbunge anayemaliza muda wake Boniface Mwita Getere.
Habari za ndani kutoka CCM Bunda zimebainisha bila kutia shaka kufanyika vikao vya ndani vya siri, kati ya Katibu huyo wa CCM Wilaya, Michael Chonya na Makatibu wa Kata ya Nyamuswa, Changwe Bita ambaye pia ndiye Katibu wa Mbunge,Cheba Genga wa Kata ya Nyamang'uta. Cheba, Mwikwabe Mahende Marwa (Macho) wa Kata ya Mihingo na JUma MIgela wa Kata ya Hunyari, Makatibu hawa na wenzao wa Kata na matawi inadaiwa wanalipwa mshahara kuanzia shilingi 150,000 hadi 300,000 na mbunge wa sasa kila mwezi.
Makatibu hao kwa umoja wao, wanapambana kuhakikisha wanalinda mishahara yao kwa kuhakikisha Mbunge aliyeko madarakani anatetea kiti chake, wakiamini pia kuwa wanasimamia uchaguzi huo kwa maslahi yao. Taarifa za ndani kutoka kwenye Kikao hicho cha siri kilichofanyika ofisini kwa Katibu huyo wa CCM Wilaya, na vingine kwa njia ya simu za mkononi zinadai azimio la kikao kilichofadhiliwa na Getere, ni kuhakikksha majina waliyoingiza yanaendelea kubaki kwenye daftari la chama na wasiruhusu majina ya wajumbe walioondolewa kurudishwa tena kwenye daftari la wajumbe kwa sababu hawamuungi mkono mbunge wao.
Ndani ya kikao hicho pia wamejadili idadi ya watia nia na wanaonyesha kuwapa wakati mgumu, kumekuwa na makubaliano ya pamoja kuhakikisha zoezi la uchaguzi ndani ya chama linasimamiwa na Makatibu wa Kata na matawi, ambao wanaamini watatumia nafasi zao kuhakikisha wajumbe ambao hawamuungi mkono Mbunge wao hawapati nafasi ya kupiga kura, au wanazuiliwa kupiga kura.
Mkakati kama huo ulitumika mwaka 2015, ambapo wajumbe halali walinyimwa haki ya kupiga kura huku wengine wakiingiza kura zaidi.
Baadhi ya wajumbe ambao majina yao yalienguliwa kwenye daftari la Chama walipolalamikia hatua hiyo, Katibu wa Wilaya Michael Chonya aliahidi kuchukua hatua za haraka kumaliza tatizo hilo.
Badala ya kusimamia majukumu yake alitoa taarifa kwa Mbunge, kuwa kuna tatizo hilo, haraka mbunge alituma kiasi cha fedha kwa viongozi wawili wa Chama (idadi ya fedha tunayo), kupitia simu zao za mikononi na kutoa maelekezo nini kisifanyike.
Ili kuonyesha kuwa ametimiza wajibu wake kusikiliza malalamiko ya wajumbe ambao majina yao yalienguliwa na Makatibu Kata kinyemera, Katibu huyo wa Wilaya alipita kwenye Kata saba za Jimbo la Bunda, akiagiza changamoto zilizojitokeza kwenye daftari la chama zirekebishwe, bila usimamizi dhabiti, akamaliza ziara yake bila kufanya marekebisho.
Baada ya Katibu huyo wa Wilaya kumaliza ziara yake kwenye Kata za Nyamang'uta, Hunyari, Mugeta, Ketare, Salama, Nyamuswa na Mihingo, ni kama alibariki uhuni, kilichofuata ni Makatibu Kata na Matawi kushindana kufuta majina ya wajumbe karibu kila Kata na matawi yake.
Miongoni mwa matawi yaliathirika zaidi ya tawi la Magunga, Kata ya Hunyari, ambako majina ya mabalozi 22 kati ya 25 wa tawi hilo walibadilishwa na kuingizwa majina ya wajumbe wasiojulikana.
Kitendo hicho kilizusha mtafaruku na sintofahamu, baadhi wakihoji inakuwaje Katibu wa Wilaya atoe maagizo ya kurekebisha kasoro huku Makatibu wa Kata na matawi waendelee kufanya mabadiliko ya majina ya wajumbe. Kufuatia vitendo hivyo Kamati ya Siasa ya tawi la Magunga, liliwasimamisha uongozi Katibu wa tawi hilo, Elisha Chandaro na Katibu Mwenezi wake.
Pamoja na kuchukuwa hatua kwa viongozi hao wa tawi, mabalozi 12, wajumbe kutoka Jumuia ya Wanawake UWT tawi na Kamati ya siasa walisafiri zaidi ya kilomita 65 kutoka Hunyari, Wilayani Bunda, kwenda Musoma mjini kwa ajili ya kufikisha malalamiko yao kwa Katibu wa CCM wa mkoa huo Iddy Mkowa, ambaye amethibitisha kuonana na wajumbe hao kutoka Kata ya Hunyari.
Baada ya kuongea na wahanga hao, Katibu wa mkoa alijaribu kumuuliza Katibu wa tawi sababu za kubadilisha majina ya wajumbe, bila hofu Katibu wa Tawi Elisha Chandaro alisema ni mpango kazi wa kulinda wapiga kura watakaomchagua Getere.
Kauli hiyo ilionekana tutokumfurahisha Katibu wa Mkoa, akaiagiza Kamati ya siasa kumchukulia hatua za kinidhamu ikiwa pamoja na kumsimamisha,
Akiongeza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kutoka Musoma, Mkowa amesema taarifa za malalamiko ya wananchi wa jimbo la Bunda kuondolewa kwenye daftari la wajumbe ziko ofisini kwake zinashughulikiwa ndani ya chama.
"kwanza nakushukuru kwa kufuatilia jambo hili. Taarifa hizo tunazo na zinashughulikiwa ndani ya chama, tunaomba ushirikiano wenu pia, kama kuna taarifa au mambo yanaenda tofauti na Chama kinavyoelekeza msisite kutujulisha tutazifanyia kazi,"alisema Iddy Mkoa Katibu wa CCM mkoa wa Mara.
Chama Cha Mapinduzi kimeelekeza kuwa mwaka huu kura za maoni zitapigwa kama ifuatavyo, mabalozi watapendekeza wajumbe wanne wa mashina, kamati za siasa matawi, kamati za utekelezaji UWT matawi, kamati za utekelezaji wazazi matawi, UVCCM matawi, mjumbe mmoja wa mkutano wa jimbo kutoka tawi, wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji, kamati za siasa Kata zote, kamati za UWT Kata zote, utekelezaji wazazi Kata zote na UVCCM Kata zote.
Wengine wanaotajwa ni wajumbe watano wa Mkutano Mkuu Jimbo na Kata, Kamati ya Siasa Wilaya, Kamati ya Utekelezaji UWT Wilaya, Kamati ya Utekelezaji Wazazi Wilaya, Kamati ya Utekelezaji UVCCM Wilaya, Sekretariet ya Wilaya, Madiwani na Wabunge viti maalumu kama watakuwepo.
Wananchi wa Jimbo la Bunda Vijijini nao wamepaza sauti kuwataka Makatibu wa Kata na matawi wa Chama hicho kuacha mara moja kubadilisha majina ya wajumbe waliopitishwa na chama mwaka 2022 kwa ajili kupiga kura za maoni za CCM kwenye uchaguzi Mkuu wa 2025.
Wamewataka wakomekufanya kitendo hicho kinalenga kuwachagulia kiongozi asiyekuwa na sifa ya kuwawakilisha kuwa mbunge wao.
Wakizungumza kwa sharti la kuhifadhi majina yao, wamesema Jimbo la Bunda Vijijini limekuwa halina Mbunge kwa zaidi ya miaka 10 kiutokana na aina ya mtu waliyemchagua kuwawakilisha.
Wengine wakimuita Mbunge wa mifukoni. Wamehoji pia kuwa tangu alipochaguliwa kuwa Mbunge mwaka 2015, hajawahi kuitisha kikao cha kusikiliza kero za wananchi.
Wananachi wanasema Jimbo la Bunda Vijijini ambalo ni masikini kuliko majimbo yote Tanzania, ambako watoto wa wakulima na wafugaji wanasumbuka kupata elimu ya juu, Mbunge waliyemtuma anatumia nafasi yake kuzuia mikopo ya wanafunzi.
Jimbo masikini mbunge anapewa dakika 10 kuwasemea wananchi wake anagawa dakika 5 kwa mbunge wa Jimbo la Serengeti ambako ndiko nyumbani kwao.
Katika hatua nyingine wana CCM kutoka Jumuia ya wazazi ya chama hicho, wamewaonya baadhi ya viongozi wao kuacha kutumia nafasi zao kupita kwa wajumbe kumfanyia kampeni mbunge isipokuwa waache demokrasia ndani ya Jumuia yao utumike.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Chama hicho, Bunda alipokuwa akihakiki taarifa za wapiga kura alinukuliwa akisema 'Mitano tena kwa Bon', jambo ambalo kama Mwenyekiti wa Jumuia hakupaswa kulisema.
Hivi karibuni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanikisha nguzo za umeme kwenye baadhi ya vijiji vya Kata ya Ketare na sehemu zingine zilizokusudiwa, mradi huo ni mpango rasmi wa serikali kuhakikisha kila kijiji kinafikiwa na nishati ya umeme mwaka 2030, tayari Mbunge amerukia ajenda hiyo akidai kuwa ndiye anasambaza hizo nguzo za umeme.
Mwananchi mmoja kutoka Bigegu amehoji kama ni yeye alikuwa wapi kwa miaka 10. Akahoji pia ni kwanini iwe sasa?.
Tags
Habari
