DAR-Wazalishaji wa mbolea na visaidizi vyake nchini wametakiwa kuhakikisha wanatunza na kuwasilisha takwimu sahihi za uzalishaji kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kupitia mfumo maalumu wa ukusanyaji wa data, ikiwa ni takwa la kusheria kama lilivyo kwenye Sheria ya Mbolea Na. 9 ya mwaka 2009 na Kanuni zake.
Kauli hiyo imetolewa Mei 28,2025 na Kaimu Meneja wa Uhamasishaji Uzalishaji wa Mbolea na Mazingira wa TFRA, Getrude Ng’weshemi, wakati akifungua mafunzo ya siku moja yaliyofanyika katika Hoteli ya Tiffany Diamond jijini Dar es Salaam.
Ng'weshemi amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa namna ya kujaza na kuwasilisha takwimu za uzalishaji zitakazosaidia kuboresha ufuatiliaji na upangaji wa mipango endelevu ya sekta ya mbolea nchini.
Alisisitiza kuwa, takwimu sahihi si hitaji la kisheria pekee, bali ni nyenzo muhimu katika kufanya maamuzi yenye tija, kufuatilia maendeleo ya viwanda, kuimarisha uwajibikaji, na kupanga mipango endelevu ya uzalishaji.
Akitoa mada wakati wa mafunzo hayo, Afisa Udhibiti Ubora kutoka Kitengo cha Usajili na Leseni, Charles Alex, amewahimiza washiriki kuhakikisha wanasajili biashara zao ili kuboresha ufuatiliaji wa bidhaa zinazozalishwa na zinazotumika nchini.
Naye, Afisa Biashara wa TFRA, Godwin Tumaini aliendesha mafunzo ya vitendo kwa washiriki, akionyesha kwa undani jinsi ya kujaza fomu maalum za uwasilishaji wa takwimu za uzalishaji.
Washiriki walipongeza juhudi za TFRA katika kuwajengea uwezo na kutoa mwongozo wa kisheria na kiutendaji katika kusimamia shughuli zao za uzalishaji na kuahidi kushirikiana kwa karibu na TFRA kwa kuhakikisha taarifa sahihi za uzalishaji zinawasilishwa kwa wakati.











