NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt.John Mduma amesema kuwa, ndani ya miaka 10 ya mfuko huo umefanikiwa kuwalipa fidia wafanyakazi na wategemezi wao wapatao 19,650 nchini.

Amesema, fidia ililipwa kwa wale ambao walipata ajali, kuugua au kufariki kutokana na kazi.
"Na hili ni hitaji la msingi la uanzishwaji wa mfuko na linaloonesha utendaji wa moja kwa moja wenye tija kwa jamii ya wafanyakazi."
Pia, amesema kwa sasa idadi ya mafao imefikia saba ambayo ni Fao la Matibabu (bila kikomo), Fao la Ulemavu la Muda Mfupi,Fao la Ulemavu wa Kudumu, Fao la Pensheni kwa Wategemezi, Fao la Wasaidizi wa Wagonjwa, Fao la Utengamao na Fao la Msaada wa Mazishi.
WCF ambayo ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Na.20 ya mwaka 2008 ambayo ilianza kutekelezwa rasmi Julai 6,2015 ni taasisi ya umma iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Pia, taasisi hiyo ipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina Na. 370 na marekebisho yake na sheria zingine zinazoongoza Ofisi ya Msajili wa Hazina, kazi na wajibu wa ofisi hiyo zimegawanyika katika makundi matatu.
Mosi, TR inawajibika kutunza hazina na rasilimali za taasisi za umma kwa niaba ya Serikali.
Pili,kuishauri Serikali kuhusu masuala ya uwekezaji na usimamizi wa taasisi za umma na mashirika yaliyoundwa kisheria.
Tatu ni udhibiti na ufuatiliaji wa utendaji wa taasisi za umma na mashirika yaliyoundwa kisheria ikiwa na jukumu la ufuatiliaji na usimamizi wa sheria.
Dkt.Mduma amesema,WCF unatoa ulinzi wa kijamii kwa wafanyakazi wote walioko katika sekta ya umma na binafsi dhidi ya madhara yanayotokana na ajali, magonjwa au vifo vinavyotokea kazini au kutokana na kazi.
Katika hatua nyingine, Dkt.Mduma amesema, mafanikio yao kwa kiwango kikubwa yamechagizwa na miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
"Mafanikio mengine tuliyopata ni WCF kutekeleza Mapinduzi ya kidijitali ambapo zaidi ya asilimia 90 ya huduma zote sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao."
Amesema, mifumo hiyo imepunguza urasimu,kuongeza uwazi na kuboresha ufanisi wa utendaji kazi.
Vilevile, Dkt.Mduma amesema,mwaka 2024 mfuko huo ulipata Cheti cha Ithibati cha ISO kwa utoaji wa huduma bora kwa viwango vya Kimataifa.
"Na mwaka 2023, mfuko ulipata Tuzo ya International Social Security Association (ISSA) kwa matumizi bora ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)."
Pia, amesema mwaka huu (2025) mfuko huo ulishika nafasi ya pili katika Tuzo za Serikali Mtandao (eGa Awards) na nafasi ya tatu kwenye TEHAMA Awards 2025 kwa taasisi za umma zilizofanikiwa kuondoa urasimu kupitia TEHAMA.
Mbali na hayo, Dkt.Mduma amesema,lengo la mfuko huo kuwekeza vitega uchumi mbalimbali nchini ni ili uweze kupata rasilimali ambazo zitawawezesha kuwa na uendelevu wa kulipa fidia kwa wanachama wake.
Tags
Habari
Kikao Kazi Msajili wa Hazina
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF)
Ofisi ya Msajili wa Hazina
WCF
WCF Tanzania