DAR-Afisa Habari na Mawasiliano wa Timu ya Mpira wa Miguu ya KenGold FC inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Bw. Joseph Emily Mkoko leo Juni 11, 2025 amehukumiwa kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya shilingi milioni moja.
Ni baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa ya kiasi cha shilingi milioni 1.5.
Makosa haya ni kinyume na kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa SURA ya 329 Marejeo ya mwaka 2024.
Awali ilidaiwa kuwa Afisa huyo alipokea rushwa kutoka kwa mchezaji mmoja wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Vital’o ya Burundi, ili amsaidie kusajiliwa na KenGold FC na kupata upendeleo wa kupangwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi,Mhe.Dkt. Beda Nyaki tarehe 30 Mei, 2025 na kufunguliwa Shauri la Jinai namba 13138/2025.
Aliposomewa mashtaka yake, mshtakiwa alikubali na kesi iliahirishwa hadi leo Juni 11, 2025 kwa ajili ya kusoma maelezo ya awali ya kosa.
Leo, mshtakiwa alikumbushwa makosa yake na kuendelea kukubali na aliposomewa maelezo ya awali ya kosa pia alikubali, hivyo mahakama imemtia hatiani.
Kesi hiyo ilikuwa inaendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Ilala, Bw. Imani Nitume.
Tags
Breaking News
Habari
KenGold FC
Mahakamani Leo
Michezo
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)