SONGWE-Mahakama ya Wilaya ya Mbozi imetoa hukumu dhidi ya Bw. Emmanuel Sambo Mgalla ambaye ni Afisa Ubora wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Mkoa wa Songwe pamoja na wenzake watatu ambao ni Afisa Manunuzi, Bw.Froicy Wilfred Mkungilwa, mlinzi Ephraim Asulumenye na mfanyabiashara Adili Sanga.
Wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha miezi sita au kulipa fidia ya shilinhi 5,500,000 na faini ya shilingi laki nane, kwa kosa la matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2022.
Kifungu hicho kikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2022.
Hukumu hiyo imetolewa katika Kesi ya Uhujumu Uchumi na 8529/2025 Juni 12, 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,Mheshimiwa Stephano Minja.
Kesi hiyo imeendeshwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Bi.Simona Mapunda.
Awali akisoma mashtaka mahakamani hapo,Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU,Bi. Mapunda alisema washitakiwa walipewa dhamana ya kusimamia manunuzi ya mahindi ya NFRA mwaka 2021, ambapo katika manunuzi hayo walitumia nyaraka kufanya manunuzi hewa ya shilingi 5,219,480.
Baada ya kufikishwa mahakamani na kusomewa makosa yaliyowakabili washitakiwa waliomba kufanya majadlilino (Plea Bargaining) na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na baada ya majadlilino ndipo walipotakiwa kulipa fidia ya shilingi 5,500,000 pamoja na faini ya shilingi 800,00.
