KIGOMA-Katika Mahakama ya Wilaya Uvinza tarehe 12 Juni, 2025 limefunguliwa shauri la jinai ECO.14247/2025 mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo,Mheshimiwa John Mtega (RM), Jamhuri dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Bi.Zainabu Suleiman Mbunda.
Wengine katika kesi hiyo ni Bashiru Fakihi Nang’uta ambaye ni Afisa Manunuzi, mfanyabiashara Salum Zuberi Kayoyo, Majid Zuberi Mabanga ambaye ni Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza pamoja na Masumbuko Hussein Kechegwa ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Maliasili.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka nane ya Matumizi Mabaya ya Mamlaka kinyume na kifungu cha 31, Ubadhirifu na ufujaji kinyume na kifungu cha 28(2),
Uchepushaji kinyume na kifungu cha 29 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya 2022, na kuisababishia hasara Serikali kinyume na Aya ya 10(1) ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa.
Inadaiwa kwamba, washtakiwa walitumia fedha za mfuko wa jimbo kwa kumpatia mshtakiwa wa tatu, kwa jina la Biashara ya Lumpungu General Supplier kiasi cha shilingi 20,850,000 kwa utekelezaji wa kazi ambazo hazikuwa zimepangwa matumizi na kamati ya fedha za mfuko wa jimbo,wala kuwepo kwa utekelezaji wa mradi kuhitaji fedha ambazo zilitolewa na kulipwa mzabuni huyo.
Aidha, washtakiwa hao walikana mashtaka yote katika shauri hilo waliyosomewa na Waendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. James Mosi Nyarobi na Bi. Mwasiti Mshana.
Washtakiwa wako nje kwa dhamana na shauri hilo litaendelea Juni 25, 2025.
