NA GODFREY NNKO
RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamo la Kitaifa la Sheria.
Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (PBA), Wakili Bavoo Junusi wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam kuelezea kuhusu kongamano hilo.
Hayo yamesemwa leo Juni 20,2025 na Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (PBA), Wakili Bavoo Junusi wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea kuhusu kongamano hilo.
Kongamano hilo linaratibiwa na chama hicho.PBA kimeanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 16A(1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura 268 na Tangazo la Serikali Na. 589 la Agosti 16, 2019.
"Lengo kubwa la kongamano hilo ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mambo mbalimbali hususani kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
"Kwa hiyo tumeona tutimize wajibu wetu ili kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya sheria. Kwa hiyo,tutachambua sheria za uchaguzi, tutazichambua moja baada ya nyingine ili wananchi waweze kuzifahamu."
Pia, amesema watajadili kuhusu masuala yanayohusiana na namna ya kutatua migogoro mbalimbali inayohusiana na uchaguzi.
Vilevile, wataelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza na kulinda amani ya nchi ikizingatiwa kuwa, kuna maisha baada ya Uchaguzi.
"Kwa hiyo ipo haja kwa wananchi, wadau na wanasiasa kulifahamu hilo, tofauti zetu hazipaswi kutugawa katika makundi. Mambo yanayotuunganisha ni mengi kuliko yale machache."
Amesema, kongamano hilo litajumuisha watu wote wakiwemo wananchi, wanasheria, wanataaluma mbalimbali, viongozi na wengine kutoka ndani na nje ya nchi bila kiingilio.


