Gavana Tutuba ashiriki Mkutano wa 32 wa Mwaka wa Benki ya Afreximbank

ABUJA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, ameshiriki katika Mkutano wa 32 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Uagizaji na Uuzaji wa Bidhaa Afrika (Afreximbank), uliofanyika mjini Abuja, Nigeria kuanzia tarehe 25 hadi 28 Juni 2025.
Mkutano huo wa kimataifa ulijadili masuala mbalimbali ya kiutendaji na kimkakati ya benki hiyo, ukiwa umebeba kaulimbiu: “Kujenga Mwelekeo katika Miongo ya Ustahimilivu”. Kaulimbiu hii ililenga kutathmini mafanikio yaliyopatikana kwa ustahimilivu wa taasisi hiyo na kujenga msingi imara wa maendeleo ya baadaye barani Afrika.

Katika mkutano huo, Gavana Tutuba alipata fursa ya kuchangia mada kuhusu "Uimara wa Taasisi za Kifedha kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika na Umuhimu wa Hadhi Maalumu ya Mkopeshaji katika Kuwezesha Utafutaji wa Fedha kwa Ukuaji wa Afrika."
Akiwasilisha mada hiyo, Gavana Tutuba alisisitiza umuhimu wa kulinda hadhi hii maalumu kwa benki za maendeleo barani Afrika, ili ziendelee kuwa na uwezo wa kupata fedha kwa ajili ya kufadhili miradi mikubwa ya kimkakati.
Alitolea mfano wa Tanzania katika utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa ya SGR, ambapo Afreximbank kwa kushirikiana na taasisi nyingine, walishiriki kikamilifu katika kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya mradi huo pamoja na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP).
Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba aliungana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, kutembelea Kituo cha Umahiri cha Matibabu ya Kibingwa cha Afrika kilichopo Abuja.

Kituo hicho ambacho kimefadhiliwa na Benki ya Afrexim kimewekwa miundombinu na vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya matibabu ya kibingwa kukabiliana na maradhi mbalimbali ikiwemo saratani.
Aidha, Gavana Tutuba alipata nafasi ya kufanya mazungumzo na mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Rais wa Benki ya Afrexim Prof. Benedict Oramah, kando ya mkutano huo, kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Benki Kuu ya Tanzania na Afreximbank.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news