NA GODFREY NNKO
WAKILI Mkuu wa Serikali,Mheshimiwa Dkt.Ally Possi ameshuhudia tukio la utiaji saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya Chama cha Mawakili wa Serikali na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Katibu wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania,Rashid Mohamed Said na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Bi.Mariam Othman wakisaini hati ya makubaliano, huku wakishuhudiwa na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi, Rais wa TLS, wakili Boniface Mwabukusi pamoja na Makamu wa TPBA, wakili Debora Mcharo.
Tukio hilo limefanyika leo Juni 13,2025 katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
Lengo la MoU hiyo ni ili kushirikiana kwa pamoja kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kubadilishana ujuzi, kutoa elimu kwa umma, kuboresha mazingira ya tasnia ili kuweza kusaidia jamii kupata haki kwa wakati.
Akizungumzia kuhusu hatua hiyo,Dkt.Possi amesema kuwa,ni njema na inalenga wanataaluma hao kushirikiana kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Pia,Dkt.Possi amezipongeza pande zote kwa kufikia hatua hiyo muhimu. "Sisi kama viongozi wa tasnia ya sheria,siku hii ni ya muhimu sana kwa vyama hivi viwili kutia saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika maeneo mbalimbali hususani maeneo ya kupeana taaluma, kwa hiyo ni muhimu kwa vyama hivi kutia saini hati hii ya makubaliano ya ushirikiano."
Amesema, kupitia ushirikiano huo mawakili wa Serikali na wale wa kujitegemea ikiwa kwa umoja wao ni maafisa wa mahakama,masuala ya usaidizi wa kisheria kwa ujumla wao wana jukumu la kulinda maslahi ya Taifa huku wakiwahudumia wananchi kwa ukamilifu.
Ameeleza kuwa,vyama hivyo viwili vitaendelea kushirikiana. "Kama tunavyosema nchi yetu inaenda katika Dira ya Maendeleo ya 2050 na katika dira hiyo kuna mambo mengi ambayo sisi kama wanasheria hatuna budi kubadilika na kuendana na dira hiyo."
Amesema, katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia kuna teknolojia nyingi zinaibuka ikiwemo Akili Unde (AI), mabadiliko ya sheria za uwekezaji na masuala mbalimbali ambayo yanaendana na wakati wa sasa, hivyo suala la kushirikiana kwa manufaa ya taifa ni jambo jema.
"Kwa hiyo hatuna budi sisi wanasheria wa nchi hii kuungana, kushirikiana, kupeana ujuzi lakini pia kushirikishana uzoefu ambapo nia sasa ni kusaidia Taifa letu katika kuhakikisha nguzo za sheria zinaimarika, lakini sheria za nchi zinaimarika.
"Lakini, miongozo ya sheria ambayo nchi yetu inasimamia iendelee kuimarika, lakini kikubwa zaidi mawakili wote, wale ambao ni wa Serikali na ambao hawapo serikalini kuhakikisha wanafaidika kwa umoja huu ambao wametia saini leo."
Aidha,amezitaka pande zote mbili kuhakikisha wanatekeleza yaliyomo katika makubaliano hayo kwa ukamilifu.
TPBA
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA), wakili Debora Mcharo amesema,mchakato huo ambao umefanikisha MoU iliyotiwa saini leo ulianza muda mrefu huku ukiwa na manufaa mengi.
"Tija na umuhimu wa makubaliano haya ni kuweza kuendeleza mashirikiano kwa sababu tunajua sisi wote ni chama cha kitaaluma, lakini tunajua TLS ni chama kikongwe, kinatujumuisha wote na sisi ni wanachama wa TLS.
"Kwa hiyo, jambo la msingi ni kuweza kutekeleza na kuweza kuelimisha jamii na Serikali yetu kuisaidia, mawakili wote wa Serikali na mawakili wa kujitegemea kufanya kazi kwa weledi na kusimamia katika misingi ya kisheria.
"Tunatambua kwamba hivi ni vyama vya kitaaluma na tuna wajibu wa kutoa elimu kwa umma katika masuala mbalimbali yanayohusu Serikali yetu na sheria za nchi yetu."
TLS
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wakili Boniface Mwambukusi amesema kuwa, vyama hivyo viwili vina majukumu yanayofanana katika kulinda Katiba, sheria na utawala bora nchini.
"Kwa hiyo maeneo mengi tunafanya cross cuting katika majukumu, kwa hiyo tunaposaini maana yake tuwe na maeneo ya ushirikiano kwa sababu bila kuwa na maeneo ya ushirikiano kuna watu labda walikuwa wanafikiria hizi taasisi ni taasisi mbili zinazoshindana.
"Hizi taasisi hazishindani, ni taasisi zinazofanya kazi bega kwa bega katika kufanikisha upatikanaji na utolewaji wa haki."Mwambukusi amesema, kuna maeneo ambayo wanatakiwa kushirikiana moja kwa moja na mengine katika kutenda.
"Lakini, kuna maeneo ni eneo la Chama cha Mawakili wa Serikali, lakini tukiwa na ushirikiano kuna namna ambayo sisi tunaweza kushirikiana ili kuwezesha kutoa mchango wetu ulio bora ambao utaisaidia Serikali na utasaidia wananchi."
Tags
Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania
Dkt.Ally Possi
Habari
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
TLS Tanganyika


