Mahakama ya Tanzania yajikita kimkakati Maonesho ya Sabasaba

NA MARY GWERA
Mahakama

MAHAKAMA ya Tanzania imeweka kambi katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), 2025 yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa huduma na elimu kwenye masuala mbalimbali ya Mahakama na sheria kwa ujumla.
Muonekano wa Banda la Mahakama ya Tanzania lililopo ndani ya Viwanja vya Mwalimu Nyerere mkabala na banda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Huduma mbalimbali ikiwemo elimu kuhusu Mahakama na Sheria kwa ujumla zinatolewa.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ushiriki wa Mahakama ya Tanzania kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), 2025, Mhe. Hussein Mushi akizungumza kuhusu ushiriki wa Mhimili huo kwenye Maonesho ya (Sabasaba).
Mmoja kati ya wananchi waliofika katika banda la Mahakama akisubiri kupata huduma kwenye Mahakama Inayotembea iliyopo ndani ya Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Sabasaba) vilivyopo barabara ya Kilwa-Temeke jijini Dar es Salaam.
Kwa mwaka huu, viongozi na watumishi wa Mahakama pamoja na wadau mbalimbali ambao ni watalaam na wabobezi katika masuala ya kisheria wanaendelea kutoa huduma na elimu ya sheria kwa muda wote wa Maonesho ambayo yameanza tarehe 28 Juni, 2025.

Katika kipindi chote cha Maonesho, Mahakama inatoa huduma mbalimbali zikiwemo za kusikiliza Mashauri kwenye Mahakama Inayotembea ‘Mobile Court Services’, kutoa Msaada wa Kisheria ‘TLS’, elimu kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mahakamani na safari ya Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.

Akizungumza katika mahojiano maalum leo 30 Juni, 2025 katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya ushiriki wa Mahakama katika Maonesho ya hayo, Mhe. Hussein Mushi ametoa rai kwa wananchi kutumia nafasi adhimu inayotolewa na Mahakama kwa kuwaleta pamoja watumishi wake na wadau katika kutoa elimu ya sheria bure na kuelimisha taratibu mbalimbali za kupata haki Mahakamani.

“Nawaomba wananchi kutumia fursa hii ya maonesho kuja kutoa maoni, malalamiko pamoja na kupata msaada wa kisheria kutoka kwa Mawakili kutoka Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanganyika (TLS), Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria pia kujua taratibu mbalimbali za Kimahakama,” amesema Mhe. Mushi.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote wa Dar es Salaam na Mikoa ya karibu kufika katika banda la Mahakama.

Huduma nyingine zinazotolewa katika banda la Mahakama ni elimu kuhusu huduma na taratibu mbalimbali za ufunguaji wa mashauri, yakiwemo mashauri ya mirathi, elimu kuhusu Mahakama ya Watoto, kuelezea manufaa au faida za Mfumo ulioboreshwa wa Kusajili, Kuratibu na Kusimamia Uendeshaji wa Mashauri (Advanced Case Management System).

Nyingine ni kutoa elimu kwa wananchi kutambua umuhimu wa kutumia Kituo cha Huduma kwa Mteja ‘Call Centre’ ya Mahakama ya Tanzania kutoa malalamiko na maoni yao.

Kueleza huduma zinazotolewa na ngazi mbalimbali za Mahakama ikiwemo Divisheni za Mahakama Kuu na Kituo cha Usuluhishi.
Idara, Divisheni na wadau mbalimbali waliopo kwenye Banda la Mahakama ya Tanzania kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), 2025.
Wananchi wakipata msaada wa kisheria kutoka kwa Mawakili wa Kujitegemea kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).(Picha na MARY GWERA, Mahakama).

Katika kipindi chote cha Maonesho hayo, Mahakama ya Tanzania ipo pamoja na baadhi ya Wadau wake ambao ni Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Chama Cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambao wote wanatoa elimu kuhusu maeneo yao.

Banda la Mahakama ya Tanzania linapatikana ndani ya Viwanja vya Mwalimu Nyerere almaarufu Viwanja vya Sabasaba na linapatikana mkabala na banda la JKT.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news