MOROGORO-Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, amewataka Watumishi wa Hazina Ndogo mkoani Morogoro kujiendeleza kimasomo ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Bi. Omolo alisema hayo wakati alipokutana na Watumishi wa Hazina Ndogo, mkoani Morogoro, ambapo pamoja na mambo mengine aliwaahidi Watumishi hao kuwa Wizara itahakikisha inaweka mazingira mazuri ikiwemo kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara ili Ofisi hiyo iweze kuwahudumia vyema Wananchi wa Mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla.
Kikao hicho cha Naibu Katibu Mkuu, kilihudhuriwa na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bi. Emma Komba, Mkuu wa Hazina Ndogo Mkoa wa Morogoro, CPA(T) Robin Kimweri, Msimamizi wa Mali za Serikali Mkoa wa Morogoro, Bw. Khamis Mouktar, Wahasibu na Wasimamizi wa Mali za Serikali na Watumishi wengine wanaohudumu katika Ofisi ya Hazina Ndogo mkoani Morogoro.




