Rais Dkt.Mwinyi azindua rasmi Kamati ya Kusimamia Madrasa Zanzibar

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameizindua rasmi Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Madrasa Zanzibar.
Ameizindua Kamati hiyo Juni 26,2025 aliposhiriki katika hafla maalum ya kuadhimisha Mwaka Mpya wa Kiislamu 1447 Hijria, iliyoambatana na dhifa ya chakula cha mchana iliyofanyika katika Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa kwa muda mrefu Madrasa zimekuwa zikikumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo mazingira yasiyoridhisha na hali duni za Walimu wa Madrasa. Hivyo, kuzinduliwa kwa Kamati hiyo kutatoa fursa ya kuweka mipango madhubuti ya kutatua changamoto hizo.
Rais Dkt. Mwinyi ameisisitiza Kamati hiyo kuandaa mpango maalum wa kuzisimamia Madrasa, ikiwemo bajeti na usimamizi wa mipango itakayoandaliwa ili kuangalia namna bora ya kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.

Vile vile, Dkt. Mwinyi amesema amefarijika na mafanikio yanayoendelea kupatikana katika taasisi zinazoshughulikia masuala ya dini ya Kiislamu katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo jitihada za utatuzi wa migogoro.

Ameipongeza Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kufanikisha ujenzi wa afisi hiyo mpya ambayo itaboresha mazingira ya kazi.

Rais Dkt. Mwinyi amewakumbusha viongozi wa dini, masheikh na wananchi kwa ujumla umuhimu wa kuiombea nchi amani, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Alhaj Dkt. Mwinyi amemkabidhi Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, Hadidu Rejea za Kamati ya Kitaifa juu ya usimamizi wa Madrasa Zanzibar.
Wakati huohuo, Rais Dkt. Mwinyi amejumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika maadhimisho maalum ya kuukaribisha Mwaka Mpya wa Kiislamu 1447 Hijria yaliyofanyika katika Msikiti wa Jammiu Zinjibar, Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news