NA LWAGA MWAMBANDE
REJEA katika Biblia Takatifu kitabu cha Mathayo 16:15-16 neno la Mungu linasema, "Yesu akawauliza, “Na ninyi je, mnasema mimi ni nani?”... Simoni Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”
Kwa muktadha huo, ni wazi kuwa majibu ya Petro yana uwanda mpana hususani kiimani.
Mtume Petro,alitambua kuwa Yesu si mtu wa kawaida tu, bali ni Kristo (Masiya) aliyeahidiwa katika maandiko, na Mwana wa Mungu aliye hai, jambo ambalo lilifunuliwa kwake na Mungu, si kwa maarifa ya kibinadamu tu.
Tunaona Mathayo 16:17,Yesu alimsifu Petro kwa ufunuo huo akasema “Heri wewe, Simoni mwana wa Yona, kwa maana si mwili na damu iliyokufunulia hili, bali Baba yangu aliye Mbinguni.”
Ni kwa msingi huo sasa,mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,kuna umuhimu mkubwa kwa mtu kujitambua au kuelewa utambulisho wake wa ndani.
Anasema,hilo ni jambo la msingi sana katika maisha ya mtu binafsi, kiroho, kihisia, kijamii na hata kimaendeleo ili kuweza kuelewa kusudi lako hapa duniani na kumtumikia Mungu kikamilifu.
Kwani,kujua wewe ni nani si suala la kibinadamu tu,bali pia ni la kiroho na mtu anayemjua Mungu ataelewa pia utambulisho wake wa kweli.Endelea;
1.Kama mtume wa Mungu, yule Paulo zamani,
Mteuliwa na Mungu, akiwapo duniani,
Alimtukuza Mungu, hata kule gerezani,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba?
2.Na Mungu alitolewa, akiwa zake njiani,
Upofu akajiliwa, bila uoni machoni,
Hadi alipopatiwa, tiba kutoka mbinguni,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba?
3.Huyu limjua Yesu, litumika duniani,
Hari kali limhusu, hata viboko mwilini,
Hayo hayakumhusu, kupasa sifa mbinguni,
Hivi mimi nani hasa nisimsifu Muumba?
4.Paulo na Sila wale, wakiwako gerezani,
Mungu limuweka mbele, kwa sifa za mdomoni,
Haikuwa ni kelele, ya kuchosha sikioni,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba?
5.Ni watumishi wakubwa, wa Mungu Baba mbinguni,
Ila ndio walikabwa, wakawekwa kifungoni,
Midomo hawakuzibwa, kupaza sifa enzini,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba?
6.Mungu ambaye hushuka, toka aliko enzini,
Sifa kwake zikifika, na kumgusa moyoni,
Kwao hao alishuka, akaingia kazini,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba?
7.Walikuwa ni mitume, watenda kazi shambani,
Mimi wala si mtume, hivi ninafanya nini,
Hawakuona utume, wa kukaa kivulini,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba?
8.Somo hili liingie, lipenye hadi moyoni,
Ufahamu unijie, humu Mwangu maishani,
Wala nisijikalie, kama niko kituoni,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba?
9.Niache kukaakaa, nami niende kazini,
Utumishi kuuvaa, kufanya ya hekaluni,
Sifa kinywani kujaa, kwa Mungu alo mbinguni,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba.
10.Halafu nilivyo huru, wala siko kifungoni,
Wala sitozwi ushuru, nyumbani hata kazini,
Mungu niangaze nuru, sifa zijae kinywani,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba.
11.Kama mitume wa Mungu, wakiwako gerezani,
Walimtukuza Mungu, akasikia enzini,
Ni vema watu wa Mungu, na sisi tuwe kazini,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba.
12.Mungu wetu mwema sana, atufaa maishani,
Wa kuabudiwa sana, kwa mema yasokifani,
Hata kumwinua sana, tukiwapo maishani,
Hivi mimi nani hasa, nisimsifu Muumba?
13.Kumtumikia Mungu, tukiwapo maishani,
Hapa tunapata fungu, wa ulinzi na amani,
Mwisho mbinguni kwa Mungu, ni milele uzimani,
Hivi mimi nani hasa nisimsifu Muumba.
(Matendo ya Mitume 16:16-36)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
