Salamu za Jumapili:Usiitwe mpumbavu

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA neno la Mungu katika kitabu Kitakatifu cha Mhubiri 10:1-3. Biblia inasema; Kama vile nzi waliokufa huharibu na kunuka katika manukato ya mtengeneza manukato, ndivyo upumbavu kidogo unavyomharibu mwenye hekima na heshima.
Picha na SS.

...Moyo wa mwenye hekima huwa upande wa kuume, bali moyo wa mpumbavu huwa upande wa kushoto.

...Naam, hata mpumbavu atembeapo njiani, moyo wake huonyesha kuwa hana akili, naye huwaambia watu wote ya kuwa yeye ni mpumbavu.

Kwa msingi huo, mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa kila mmoja wetu anahitajika kuwa mwaangalifu hata kwa mambo madogo.

Ni kwa sababu dhambi ndogo zinaweza kuzima harufu nzuri ya manukato ya maisha ya utakatifu.

Rejea Luka 16:10 neno la Mungu linasema,mtu ambaye ni mwaminifu katika mambo madogo, atakuwa mwaminifu hata katika mambo makubwa na mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo hatakuwa mwaminifu katika mambo makubwa.Endelea;

1. Unapaswa kusamehe, usijedharauliwa,
Vile wasiosamehe, hukosa kuheshimiwa,
Ni laana si sherehe, sifa ile wanapewa,
Achilia msamaha, usiitwe mpumbavu.

2. Kweli amekukosea, hilo tunalielewa,
Kinyongo kuendelea, kwa huyo mtuhumiwa,
Nyongo unajiwekea, na hasira kuzidiwa,
Achilia msamaha, usiitwe mpumbavu.

3. Haraka kukasirika, rohoni unaambiwa,
Kifua inakishika, wahemewa mkosewa,
Kwa Mungu dharaulika, kichwa ngumu kuelewa,
Achilia msamaha, usiitwe mpumbavu.

4. Unazidi jikosea, endapo umekosewa,
Hasira zaendelea, kifuani wapaliwa,
Ni gizani wapotea, tena wadharauliwa,
Achilia msamaha, usiitwe mpumbavu.

5. Una akili timamu, haujachanganyikiwa,
Ukurudi ufahamu, hayo uliyotendewa,
Kwamba ni ubinadamu, kukosa na kukosewa,
Achilia msamaha, usiitwe mpumbavu.

6. Ukiitwa mpumbavu, jua wewe sawasawa,
Na wale watu wachovu, Mungu wasiomwelewa,
Ambao kwao wokovu, kitu chadharauliwa,
Achilia msamaha, usiitwe mpumbavu.

7. Mpumbavu amesema, kwa Neno tunaambiwa,
Mungu hayupo kahama, kwamba mwenye anatawa,
Ni ujinga na ujima, dhahama atajiliwa,
Achilia msamaha, usiitwe mpumbavu.

8. Kama ukiachilia, msamaha sawasawa,
Hapo unafungulia, na wewe kuachiliwa,
Uliyojitibulia, Mungu atakuelewa,
Achilia msamaha, usiitwe mpumbavu.
(Mhubiri 7:9, Mathayo 6:12)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news