DODOMA-Katika juhudi za kulinda watumiaji wa huduma za fedha dhidi ya manyanyaso ya kifedha na kuhakikisha haki na usawa katika sekta ya fedha, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amezindua mfumo mpya wa kushughulikia malalamiko ya wateja wa SEMA na BoT pamoja na Mazingira ya Majaribio ya Teknolojia ya Fedha, katika hafla iliyofanyika Juni 5, 2025 jijini Dodoma.

Amesema, mikopo hiyo imekuwa chanzo cha mateso kwa wananchi wanaotafuta mikopo ya haraka huku wakikwepa taasisi rasmi za kifedha.
“Kuzinduliwa kwa mfumo wa SEMA na BoT kutaongeza imani ya umma katika kutumia huduma rasmi za fedha na kuboresha uwajibikaji kwa watoa huduma za fedha wanaosimamiwa na Benki Kuu,”alisema.
Dkt. Nchemba ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuandaa mfumo unaojibu moja kwa moja changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi, na kuutaja kama utekelezaji wa dhahiri wa falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya 4R kwa kuleta mageuzi katika huduma za fedha.
Kwa upande wake, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema mfumo wa Sema na BoT ni wa kidigitali na utamwezesha mtumiaji wa huduma za fedha kuwasilisha malalamiko kwa njia ya tovuti, simu janja kupitia programu tumishi (Apps), na hata kwa simu za kawaida kupitia USSD.
“Mfumo huu ni rafiki na utamuwezesha kila mtumiaji wa huduma za fedha kuufikia na kuutumia wakati wowote, bila kujali mahali au uelewa wa teknolojia," alisema.
Aidha, Gavana Tutuba amesema kuwa mfumo huo utawezesha taasisi za fedha kubaini na kushughulikia malalamiko ya wateja kwa haraka, pamoja na kukusanya takwimu za malalamiko yaliyowasilishwa na kushughulikiwa. Takwimu hizo zitatumika kama nyenzo muhimu kwa taasisi za fedha katika kuboresha huduma zao na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wateja.
Katika hatua nyingine, Benki Kuu kupitia Wizara ya Fedha imezindua Mazingira ya Majaribio ya Teknolojia ya Huduma za Fedha (Fintech Regulatory Sandbox) kwa lengo la kutoa fursa kwa wabunifu kujaribisha bidhaa na huduma mpya za kifedha chini ya usimamizi wa karibu wa Benki Kuu.
Dkt. Mwigulu alisema kuwa hatua hiyo itaongeza kasi ya ubunifu na kuchochea matumizi ya teknolojia kama vile blockchain, AI, huduma za malipo kidigitali, mabenki mtandao, ubadilishaji fedha za kigeni na hata uwekezaji kwenye sarafu mtandao (cryptocurrency).
“Teknolojia ya fedha ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla. Ni wazi kuwa Tanzania iko kwenye njia sahihi ya kujenga uchumi shindani, jumuishi na wa kisasa,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa BoT (Uthabiti wa Sekta ya Fedha), Bi. Sauda Msemo, amesema kuwa mfumo wa Sema na BoT pamoja na Mazingira ya Majaribio ya Teknolojia ya Fedha ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha (2023–2028) na Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (2020/21–2029/30).
Hatua hii mpya ya serikali na Benki Kuu ni ushahidi wa dhamira thabiti ya kujenga uchumi jumuishi, ambapo kila Mtanzania, popote alipo, anaweza kupata huduma bora za kifedha kwa haki, usalama na ufanisi.