ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika sekta ya michezo kwa kujenga viwanja vya kisasa.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Juni 18,2025 alipokutana na Wajumbe wa Kamati ya Michezo ya Majeshi ya Tanzania (BAMATA) waliomtembelea Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.
Amesema, Serikali imeamua kuwekeza katika michezo kutokana na kutambua umuhimu wake katika kukuza uchumi, kutoa fursa za ajira, na kuimarisha afya ya jamii.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza BAMATA kwa mafanikio makubwa ya kuandaa mashindano ya majeshi kila mwaka, na ametumia fursa hiyo kupendekeza mashindano ya mwaka huu yafanyike Zanzibar, kutokana na kuwepo kwa viwanja vya kutosha kwa michezo mbalimbali.
Amesema kuwa hatua hiyo pia ni fursa muhimu ya kuitangaza Zanzibar katika ngazi ya kitaifa.
Ameongeza kuwa kufanyika kwa mashindano hayo visiwani kutadhihirisha ushirikiano wa karibu baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na vikosi vya ulinzi na usalama nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Serikali, kupitia taasisi zake za umma pamoja na kushirikiana na sekta binafsi, itatoa mchango wake katika kufanikisha mashindano hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania, Brigedia Jenerali Said Khamis, ameeleza kufarijika na maendeleo makubwa ya ujenzi wa viwanja vya michezo Zanzibar hatua ambayo itakayosaidia kufanikisha mashindano ya mwaka huu kwa ufanisi mkubwa.
Amesema Kamati inatambua juhudi za Rais Dkt. Mwinyi katika kuboresha miundombinu ya michezo na imeridhia ombi lake la kufanikisha mashindano ya mwaka huu kufanyika Zanzibar. Ameeleza kuwa hatua hiyo itatoa taswira nzuri kwa wananchi kuhusu ushirikiano uliopo kati ya SMZ na Vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Mashindano ya Majeshi yanatarajiwa kuanza tarehe 14 Agosti 2025 Zanzibar.