Mnyororo wa Ugavi unalenga kutimiza matarajio ya kupata huduma toshelevu-Dkt.Mwasimba

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha imesema kuwa, mnyororo wa ugavi unalenga kutimiza matarajio ya kupata huduma toshelevu na kwa wakati huku thamani halisi ya fedha zilizotumika katika shughuli za mnyororo huo ikipatikana.
Hayo yamesemwa leo Juni 18, 2025 mkoani Morogoro na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dkt.Maige Mwasimba wakati akitoa mada kuhusu masuala ya usimamizi wa mnyororo wa ugavi katika sekta ya umma katika semina kwa wamiliki na waandishi wa vyombo ya habari mitandaoni.

Semina hiyo iliyoratibiwa na Wizara ya Fedha imefunguliwa na Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Dkt. Frederick Mwakibinga kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, katika ukumbi wa Mikutano wa 88 mkoani hapa.

“Vitu na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa duniani, si lazima ziwe zinatumika zinapozalishwa, kinachowezesha sisi kupata huduma hizo ni mnyororo wa ugavi, kwa sababu tunashirikiana katika upatikanaji wa bidhaa katika mfumo huo.”
Dkt.Mwasimba amesema kuwa, myororo wa ugavi ni mtangamano wa shughuli za ununuzi,ugomboaji na uondoshaji.

Pia, unajumuisha shughuli za upokeaji, urejeshaji, utunzaji, uhifadhi na matumizi, usambazaji wa bidhaa,vifa au mali za umma.

Dkt.Mwasimba amefafanua kuwa, kupitia mnyororo wa ugavi kuna faida mbalimbali ikiwemo ongezeko la ajira kupitia ushirikishwaji jumuishi wa wananchi wazawa katika utekelezaji wa shughuli za myororo huo.

Amesema, ongezeko la ajira huwa linapatikana kwa sababu mfumo huwa unahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo ununuzi, uhifadhi, upakiaji,usafirishaji na usambazaji wa bidhaa.“Hivyo, huhitaji nguvu kazi ya kutosha katika kila hatua.”
Faida nyingine, Dkt.Mwasimba amesema, ni ujumuishi ambao unawajengea uwezo wananchi kupitia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mnyororo wa ugavi.

Amesema, kupitia ushirikiano huo huruhusu kuhamisha ujuzi,teknolojia na mbinu bora za kazi kutoka kwa wadau wa sekta binafsi kwenda kwa wananchi katika shughuli mbalimbali za ugavi.

Vilevile, Dkt.Mwasimba amebainisha kuwa, kupitia mnyororo wa ugavi, sekta binafsi inashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa shughuli za ugavi.

“Mnyororo wa ugavi unahitaji weledi,miundombinu na teknolojia bora ambayo mara nyingi hupatikana kupitia sekta binafsi,hivyo kuwavutia kushiriki moja kwa moja katika utoaji wa huduma.”
Ameongeza kuwa, ushiriki huo huwa unachochea ubunifu,ufanisi, uwekezaji wa rasilimali zaidi, hivyo kuongeza tija na uendelevu wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Faida nyingine, Dkt.Mwasimba amesema ni uzingatiaji wa uhifadhi wa mazingira na kusaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema, faida hiyo inapatikana kupitia matumizi ya mbinu endelevu ikiwemo usafirishaji rafiki kwa mazingira.
Pia,amesema mnyororo wa ugavi unasaidia kupunguza matumizi ya vifungashio visivyoharibika kirahisi na utekelezaji wa sera za ununuzi zinazozingatia bidhaa zenye atahari ndogo katika mazingira.

“Kupitia mnyororo wa ugavi unaozingatia mazingira , taasisi na wadau wake wanaweza kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, kutumia nishati mbadala na kupunguza taka.
“Hivyo kuchangia katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda rasilimaliza asili kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news