Serikali ya Awamu ya Sita yaendelea kuimarisha Sekta ya Mifugo kwa vitendo

SIMIYU-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahimiza wafugaji nchini kushiriki kikamilifu katika Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo ili kulinda afya ya mifugo yao, kuongeza uzalishaji na kufungua fursa zaidi za biashara ya mifugo katika soko la ndani na nje ya nchi.
Akizindua kampeni hiyo Juni 16,2025 Rais Dkt.Samia amesema Serikali itagharamia nusu ya gharama za chanjo na utambuzi kwa lengo la kumuwezesha mfugaji mdogo kupata huduma bora kwa bei nafuu na aliongeza kuwa Serikali itabeba gharama zote za uwekaji wa hereni kwa mifugo ili kupata takwimu sahihi zitakazowezesha kupanga na kusimamia sekta hiyo kwa tija zaidi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akizindua Mpango wa Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kitaifa kwa mwaka 2024/25- 2028/29 katika viwanja vya Nanenane Bariadi, mkoani Simiyu, tarehe 16 Juni, 2025.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa pamoja na Tanzania kuwa na idadi kubwa ya mifugo,mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa bado ni mdogo kutokana na changamoto za magonjwa, ukosefu wa takwimu na miundombinu hafifu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt, Samia Suluhu Hassan akikabidhi Pikipiki na Vishikwambi kwa maafisa mifugo kwaajili ya kurahisisha Shughuli za kuwahudumia wafugaji Nchini wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo pamoja na Kilele Cha Kongamano la Wafugaji 2025 Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu Juni 16,2025.
Vilevile, Rais Dkt. Samia ameielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka utaratibu maalum utakaowezesha zoezi la utambuzi wa mifugo kuwa endelevu na kufikia maeneo yote nchini na amesema kuwa chanjo zote zitakazotumika kwenye kampeni hiyo zitazalishwa hapa hapa nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza mara baada ya kufungua kiwanda cha kutengeneza mabomba ya maji na uchakataji wa pamba cha MOLI Oil Mills Co. Ltd kilichopo Bariadi Mkoani Simiyu tarehe 16 Juni, 2025.
Aidha, Rais Dkt. Samia amezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo utakaotumika kama rejea kwa viongozi wa maeneo yote, wataalamu wa mifugo na wadau wa sekta binafsi katika kusimamia na kufanikisha kampeni hiyo.

Hali kadhalika, Rais Dkt. Samia amepongeza ushirikiano baina ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na makampuni ya ndani katika uzalishaji wa chanjo, hatua inayopunguza gharama za uagizaji chanjo kutoka nje na kuimarisha uwezo wa taifa kudhibiti magonjwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akifungua kiwanda cha kutengeneza mabomba ya maji na uchakataji pamba cha MOLI Oil Mills Co. Ltd kilichopo Bariadi Mkoani Simiyu tarehe 16 Juni, 2025.
Pamoja na hayo, Rais Dkt. Samia ameziagiza mamlaka za Serikali kuhakikisha viwango vya
ubora, usalama na ufanisi wa chanjo zinazozalishwa kabla ya kusambazwa kwa wafugaji.

Rais Dkt. Samia pia amesema hatua zinazochukuliwa hivi sasa, ikiwemo uanzishaji wa kanzidata ya kitaifa ya kilimo na mifugo, zinaanza kuleta mabadiliko chanya katika kupanga mipango ya kisekta, kufungua fursa za uwekezaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania kimataifa.

Rais Dkt. Samia pia amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta
binafsi kushiriki katika kuendeleza mifumo ya uzalishaji, huduma na masoko ya mifugo kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali kupitia ubunifu wa kiteknolojia na huduma rafiki kwa mfugaji wa kawaida.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mkurugenzi wa Kiwanda cha MOLI Oil Mills Co. Ltd Milembe Gugu Silanga kuhusu utengenezaji wa mabomba ya maji na uchakataji wa pamba kabla ya ufunguzi wa kiwanda hicho Bariadi mkoani Simiyu tarehe 16 Juni, 2025.
Mapema, Rais Dkt. Samia alianza ziara yake mkoani Simiyu kwa kuzindua kiwanda cha kutengeneza mabomba ya maji na kiwanda cha kuchakata pamba vinavyomilikiwa na Kampuni ya NGS Tanzania Ltd.

Katika kuimarisha utawala bora, alizindua rasmi majengo mapya ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, na Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Simiyu.
Muonekano wa Kiwanja cha MOLI Oil Mills Co. Ltd kiwanda cha utengenezaji wa mabomba ya maji na uchakataji wa pamba kilichopo Bariadi mkoani Simiyu tarehe 16 Juni, 2025.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amefungua rasmi Shule ya Sekondari ya Wasichana ya mchepuo wa Sayansi ya Mkoa wa Simiyu, ambapo amesisitiza uwekezaji wa Serikali katika kuhakikisha watoto wa kike wanapata fursa zaidi ya kusoma masomo ya sayansi ili kuimarisha mchango wa wanawake katika ujenzi wa Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news