Mahujaji waipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepongezwa kwa hatua yake ya kuandaa utaratibu mzuri uliorahisisha safari ya waumini wa Kiislamu waliokwenda Makka Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Hijja mwaka huu.
Mwenyekiti wa taasisi ya Khairat Hajj & Umrah Al Hajj Suleiman Rashid, amesema juhudi za serikali ziliisaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa mahujaji unafuu na wepesi wa safari yao kutoka Zanzibar hadi katika mji wa Madina.

Akizungumza baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Sheikh Abeid Amani Karume wakitokea nchini Saudi Arabia, alisema utaratibu huo uliopangwa na serikali kwa kutayarisha ndege maalumu ya shirika la Saudia Airline kuwapeleka mahujaji wa Zanzibar moja kwa moja hadi mji mtakatifu wa Madina na kuwarejesha Zanzibar, uliwapunguzia uchofu na kuwapa utulivu wa nafsi na miili.

"Tunaishukuru sana serikali yetu ya Zanzibar kwani jitihada zake zilituwezesha kutekeleza vizuri ibada ya Hijja na sote tumefurahi kwa hilo tukitaraji utaratibu huu utakuwa endelevu In Sha Allah,” alieleza Mwenyekiti huyo.

Katika hatua nyengine, Al Hajj Rashid alitoa wito kwa Waislam kutia nia na kujiandaa kufanya ibada hiyo ambayo ni fursa ya kuvuna neema zinazopatikana katika miji mitakatifu ya Makka na Madina na kujiandalia hatma njema baada ya maisha ya duniani.

Baadhi ya mahujaji waliowasili katika uwanja huo walitoa wito kwa Waislamu waliofanikiwa kutekeleza ibada hiyo kuzitunza hijja zao kwa kuendeleza matendo mema kwa kufuata maamrisho ya dini yao na kujiepusha na makatazo yake.

Mmoja wa waratibu wa jumuiya ya Khairat Hajj & Umrah Hajjat Mwanakheri Maulid Hamad, aliwashauri vijana kufanya ibada hiyo wakiwa na nguvu zao ili kuitekeleza ipasavyo.

Mbunge wa jimbo la Chumbuni Ussi Salum Pondeza akiwa miongoni mwa wananchi waliokwenda kuwapokea Mahujaji hao, aliwapongeza kwa uthubutu na kuwaombea dua Waislamu wengine ambao bado hawajahiji wapate uwezo wa kutekeleza nguzo hiyo ya tano ya dini ya Kiislamu.

Jumla ya mahujaji 290 waliokuwa katika mjumuiko wa taasisi tano zinazoandaa safari ya Hijja, waliwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume wakirejea Zanzibar baada ya kukamilika kwa ibada hiyo inayomuwajibikia kila Muislamu mwenye uwezo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news