SMZ yajipanga kuimarisha usimamizi na ukusanyaji wa mapato

ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuimarisha usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali nchini.
Kauli hiyo ameitoa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Dkt. Saada Mkuya Salum wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani.

Amesema, Serikali imekuwa ikichukuwa hatua maalum za kuweka utulivu wa mfumo wa kodi nchini ikiwa ni njia ya kuimarisha mazingira ya biashara, kushajiisha uwekezaji na ulipaji kodi kwa hiari.

Amesema,wataimarisha uzalishaji wa Viwanda vya ndani na kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Namba 8 ya Mwaka 2017 pamoja na marekebisho katika Sheria ya Usafiri Baharini Zanzibar Nam. 5 ya 2006 kwa kuweka sharti la kuwasilisha cheti cha uthibitisho wa ulipaji wa kodi wakati wa usajili wa vyombo vya baharini.

Amefahamisha kuwa,wataweka utaratibu maalum wa usajili wa vyombo vya moto kwa kuzingatia aina ya chombo husika, kwa kuweka tofauti ya namba za usajili kwa vyombo vya maringi manne, matatu na mawili ili kudhibiti na kuvitambua kwa haraka.

“Kwa mwaka wa fedha uliopita 2024/25 Serikali ilitoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 120 kwa uingizaji wa shisha ili kuwalinda vijana ambao ndio nguvu kazi kwa taifa. 

"Hata hivyo, bado kumekuwa na wimbi kubwa la ongezeko na matumizi ya bidhaa hizo nchini, hali ambayo imepelekea matumizi ya bidhaa hiyo kuongezeka kwa vijana. 

"Hivyo inapendekezwa kutoza kiwango maalum (specific rate) cha ushuru wa bidhaa cha TZS 28,232 kwa uingizaji wa kilo moja ya ladha ya shisha (flavoured sheesha) ili kupunguza matumizi ya bidhaa hiyo kwa vijana,” ameeleza Dkt. Mkuya.

Hata hivyo Waziri saada amefahamisha kuwa Serikali itafanya mapitio na marekebisho katika Sheria za kodi na misamaha ili kuimarisha usimamizi na ukusanyaji wa Mapato ya Serikali pamoja na kuweka mkakati maalum wa matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato kwenye Wizara na Taasisi za Serikali.

Waziri Saada ameliomba baraza hilo tukufu liidhinishe TZS 6,982.076 bilioni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news