DODOMA-Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesaini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu na kampuni za uchimbaji madini pamoja na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita (GGR).
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika leo Juni 16, 2025 katika Ukumbi wa Kambarage uliopo Wizara ya Fedha jijini Dodoma, na kushuhudiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, pamoja na Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde.Waziri Dkt.Nchemba amesema, hatua hiyo ni utekelezaji wa Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, kinachowataka wachimbaji kuuza asilimia 20 ya uzalishaji kwenye masoko ya ndani, ikiwemo Benki Kuu yenye haki ya kwanza ya ununuzi wa dhahabu.
Amesema, hatua hiyo itaongeza akiba ya fedha za kigeni na kusaidia viwanda vya usafishaji dhahabu nchini kupata ithibati ya kimataifa ya LBMA.
Alibainisha kuwa hadi sasa BoT imenunua tani 5 za dhahabu zenye thamani ya dola milioni 554, zaidi ya lengo la dola milioni 350 kwa mwaka 2024/25.
“Hii ni hatua ya kihistoria kwa sababu inahakikisha dhahabu inasafishwa hapa nchini na kutunzwa kama sehemu ya akiba ya taifa,” alisema Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa lengo la BoT ni kununua tani 6 kwa mwaka wa fedha 2024/25, huku akitoa wito wa kuendeleza mkakati huu wa kitaifa kwa kuwa bei ya dhahabu imeendelea kupanda kimataifa.
Naye, Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, alisema mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 9.0 mwaka 2015 hadi 10.1 mwaka 2024/25.Mapato kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali yameongezeka kutoka Sh. bilioni 162 hadi Sh. bilioni 753, lengo likiwa ni kufikia Sh. trilioni 1.







