NA GODFREY NNKO
SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha imesema kuwa,hadi kufikia Aprili 2025, jumla ya shilingi
trilioni 10.19 zimelipwa kwa notisi za madai ya deni lililoiva la Serikali sawa na asilimia 84.8 ya lengo la mwaka.
Waziri wa Fedha,Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ameyasema hayo leo Juni 4,2025 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025|2026.
Amesema,kati ya kiasi hicho,jumla ya malipo ya deni la ndani ni shilingi trilioni 6.01 ambapo riba ni shilingi trilioni 2.48 na mtaji shilingi trilioni 3.53 na deni la nje ni shilingi trilioni 4.18 huku riba ikiwa ni shilingi trilioni 1.62 na mtaji shilingi trilioni 2.56.
Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Nchemba amesema,wizara yake imefanya maboresho ya Mfumo wa Usimamizi wa Takwimu za Madeni (CS Meridian) na kuunganishwa na mifumo mingine ya usimamizi wa fedha za umma ikiwemo Mfumo wa Benki Kuu ya Tanzania (CBS, GSS) na Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE).
"Hatua hii imeiwezesha serikali kutoa taarifa za deni la serikali kwa shilingi ya Tanzania kwa
wakati na kwa usahihi."
Makusanyo mwakani
Wakati huo huo, Waziri Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kukusanya jumla ya shilingi trilioni 34.10 katika mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwa ni mapato ya kodi na yasiyo ya kodi.
Ameeleza kuwa, kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 32.31 zinatarajiwa kutokana na mapato ya kodi, huku trilioni 1.79 zikitarajiwa kutoka kwenye vyanzo visivyo vya kodi.
Waziri Dkt.Nchemba ameongeza kuwa, TRA itaendelea kuboresha mifumo ya usimamizi wa mapato kwa njia ya kielektroniki kama vile TANCIS na IDRAS, sambamba na kuimarisha utoaji wa elimu ya kodi kwa umma.
“Kupitia maboresho haya, tunalenga kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato, kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kupunguza mianya ya upotevu wa mapato inayotokana na udanganyifu wa taarifa za miamala na biashara za magendo."
Vilevile,Waziri Dkt.Nchemba amesema, wizara yake inaendelea kuimarisha na
kuboresha mifumo ya usimamizi wa mali za serikali ikiwemo kuhamisha kanzidata mbili (GeRAS na GAMIS Portal) kwenda kwenye teknolojia ya chanzo huria (Open- Source).
Amesema,lengo ni kupunguza gharama za uendeshaji wa mifumo,kuongeza usalama, kuimarisha udhibiti wa teknolojia na
kuondoa utegemezi katika uendeshaji wa mifumo.
Dkt.Nchemba amesema kuwa,wizara kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania imekamilisha kazi ya maboresho ya Mfumo wa Usimamizi wa Forodha (TANCIS) pamoja na ujenzi wa Mfumo wa Kodi za Ndani (IDRAS) ambapo huduma za magari na leseni za udereva zimeanza kutolewa kupitia mfumo huo.
"Mifumo hiyo itasaidia kuongeza mapato ya serikali, ambapo shughuli zote za
ukadiriaji wa kodi zitafanywa kwa usahihi kupitia mfumo huo na hivyo kuondoa urasimu, kuongeza uwazi na uwajibikaji."
Majukumu ya wizara
Wizara ya Fedha na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 619A la tarehe 30 Agosti 2023.
Majukumu hayo ni pamoja na kubuni na kusimamia utekelezaji wa sera za uchumi jumla, fedha,ununuzi wa umma na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi,kuandaa na kusimamia miongozo na utekelezaji wa bajeti ya serikali.
Pia,kuratibu upatikanaji wa fedha na kuimarisha uhusiano na taasisi za kifedha za kikanda na kimataifa,kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi,kusimamia ulipaji wa mafao na pensheni kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina.
Vilevile,kusimamia fedha na mali za serikali,
kusimamia deni la serikali,kusimamia masuala ya pamoja ya fedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,kusimamia maendeleo
ya sekta ya fedha na kusimamia takwimu rasmi za kitaifa.
