SGR licha ya kuokoa muda, yafungua fursa za ajira na maduhuli ya Serikali

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema,uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya usafirishaji wa reli ya kisasa umeanza kuleta matunda huku ukifungua fursa mbalimbali za ajira.
"Mheshimiwa Spika, kwa upande wa reli, nililiahidi Bunge hili kuwa tutakamilisha ujenzi wa reli ya Dar es Salaam hadi Dodoma na kuendelea na ujenzi wa vipande vingine.

"Ninafurahi kusema kuwa awamu mbili zimeshakamilika na huduma kwa njia ya reli ya kisasa (SGR) kwa kipande cha Dar es Salaam - Morogoro-Dodoma zimeanza."

Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Juni 27,2025 wakati wa hotuba ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

Amesema,tangu safari za abiria zianze mwezi Agosti mwaka 2024, tayari jumla ya abiria 2,054,828 wamesafiri na maduhuli ya shilingi bilioni 60.88 yamekusanywa.

Pia,amesema kuanza kwa huduma za usafiri kwa reli hiyo kumeongoza tija kwenye uchumi, kwani kumefupisha safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka saa 8 hadi 9 kwa gari hadi wastani wa saa 3.

"Sasa, imekuwa kawaida mtu kuamka Dar es Salaam, kusafiri kuja Dodoma kwa reli kufanya shughuli zake na kisha kurejea Dar es Salaam jioni. Hii ni hatua kubwa katika maendeleo ya nchi yetu."

Vilevile amesema,ujenzi wa vipande vingine vya SGR unaendelea ambapo kipande cha kutoka Mwanza - Isaka (km 341) umefikia asilimia 63.16; Makutupora - Tabora (km 368) umefikia asilimia 14.53;

Tabora - Isaka (km 165) umefikia asilimia 6.65; na Tabora - Kigoma (km 506) umefikia asilimia 7.81.

Aidha, maandalizi ya kuanza ujenzi wa kipande cha Uvinza - Malagarasi - Musongati (Km 282) kinachounganisha Tanzania na Burundi yameanza na tunatarajia kuzindua ujenzi hivi karibuni.

"Kutekelezwa kwa mradi huu wa SGR, kumezalisha ajira 9,376 pamoja na kampuni zaidi ya 792 za Watanzania kusaini mikataba kwa ajili ya kandarasi na huduma mbalimbali."

Amesema, Serikali pia imenunua mabehewa ya mizigo 264 ambapo kazi ya majaribio ya mifumo imefanyika.

"Ninafurahi kulijulisha Bunge hili kwamba, leo ni siku ya kihistoria kwenye reli yetu ya SGR kwa kuwa Shirika la Reli limeanza rasmi safari za mizigo kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma.

"Tunatarajia hatua hii ya kimageuzi nchini itapunguza muda na gharama ya uchukuzi, kuchochea biashara, na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara la Afrika Mashariki."

Rais Dkt.Samia amesema,Serikali inaendelea na uboreshaji wa reli ya kati iliyokuwepo awali, yaani Metre Gauge Railway au MGR, ambayo inaendelea kutoa huduma kwa njia ya Kati na Kaskazini sambamba na reli ya SGR.

Katika kutekeleza azma hiyo, amesema wamenunua vichwa vya treni vitatu, mabehewa ya abiria 22 na ya mizigo 44 na mabehewa 350 ya mizigo na 33 ya abiria yamekarabatiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news